BARAZA la kitaifa la makanisa nchini Kenya kwa mara nyingine limeonesha wasiwasi wao kwa uongozi wa rais Ruto kwa kile wanamshutumu kiongozi wa taifa kwa kuendekeza uongo.


Katika mkutano na waandishi wa habari Jumanne, baraza la NCCK lilisema kwamba katika uongozi wa Ruto, uongo umeendekezwa na kutukuzwa kiasi kwamba wananchi hawajui ni kipi cha kuamini tena.


Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

“Uongo na kudanganya vimetukuzwa kiasi kwamba hakuna yeyote anayejua ni nini cha kuamini tena. Hekaya hizi mara nyingi zimejikita kwenye uongo na udanganyifu,’ alisema Elias Otieno, mwenyekiti wa NCCK.


Mwenyekiti huyo aliendelea mbele kwa kuwarai wananchi kujitokeza na kutafuta ukweli.


“Tunatoa rai kwenye Wakenya, ndugu na dada kuutafuta ukweli,” aliongeza.


Kwa upande wake, katibu mkuu wa NCCK, Chris Karanja, alisema kwamba ni wakati umefika sasa kutumia madaraka ya ofisi ya mwananchi, moja yao ikiwa ni kuzungumza na kusimamia ukweli.


“Tunawaomba wachungaji popote walipo, kuzungumza kwa ukakamavu, na kuhubiri bila vikwazo na pia kutoa unabii wakati Mungu amewapa ufunuo,” Karanja aliwarai wachungaji.


Baraza hilo pia lilisema kwamba wanasiasa hawatakuwa wanaruhusiwa kuzungumza kanisani wakati wa ibada.


“Watu wote wako huru kuhudhuria ibada za kanisa na kutoa sadaka zao. Lakini hatutakubali maeneo matakatifu kutumika kwa kujinadi binafsi kwa wanasiasa.”


“Tutaendelea kupalilia na kutumia maelekezo yaliyotolewa na NCCK ambayo yanatutaka kutowaruhusu wanasiasa kuhutubia wuamini ndani ya kanisa,” alisema askofu mkuu wa kanisa la Ack, Jackson Ole Sapit.


Wakati uo huo, NCCK wametishia kuongoza maandamano iwapo tume ya uchaguzi na mipaka IEBC haitabuniwa kwa kuteuliwa kwa makamishna na mwenyekiti.


Tangu kukamilika kwa muhula wa tume ya uchaguzi na uratibu wa mipaka IEBC mnamo Januari mwaka 2023, tume mpya ya IEBC yenye jukumu la kuendesha uchaguzi mkuu nchini ingali kubuniwa licha ya baadhi ya maeneo bunge na wadi nchini zikikosa uwakilishi kutokana na kufariki kwa viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi wa 2022 na katika sehemu nyingine, mahakama ikifutilia mbali ushindi wa viongozi waliokuwa wametangazwa na IEBC.