WAKILI anayewakilisha kisheria mchungaji mwenye utata wa kanisa la Good News International huko Shakahola kaunti ya Kilifi, Paul Mackenzi amepuuzilia mbali tetesi zinazoendeshwa mitandaoni kwamba ameaga dunia.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mombasa Jumatatu, wakili Lawrence Obonyo alitaja taarifa za kifo cha mteja wake kama propaganda mbaya, akisisitiza kwamba Mackenzie yuko hai na buheri wa afya.

 “Huu uvumi hatujui sababu yake lakini tunaweza tu kushuku kwamba pengine mtu Fulani mahali Fulani ana lengo hasi lakini ili kunyoosha maelezo, pasta Paul Mackenzi yu hai na buheri wa afya kabisa. Lengo lake ni kuendelea kupigana dhjidi ya hii kesi na pia kupigania jina lake na tunaomba sana kwamba kitu chochote kisimfanyikie wakati wa kesi hii,” wakili Obonyo alisema.


Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans


Obonyo aliwataka wale wanaoendesha na kusambaza uvumi huo kukoma mara moja.

“Kwa yeyote anayeeneza uvumi huu nakuomba kwa unyenyekevu kwamba ukome na uzingatie hali ya waathirika hapa ambao ni watoto lakini pia uzingatie maslahi ya umma kwa jumla ambao wana hamu ya kutaka kujua hatima ya kesi hii. Lakini pia angalia familia za wale wanaotuhumiwa kwa sababu sheria inasema kwamba washukiwa wanasalia kuwa bila hatia hadi pale watakapopatikana na hatia,” wakili huyo aliomba.


Paul Mackenzie anatuhumiwa kuhusika na vifo vya zaidi ya waumini wa kanisa lake 400 ambao anaarifiwa kuwashawishi kujitesa njaa hadi kufa kama njia ya kumuona Mungu.


Wakati uo huo, wakili huyo aliiomba ofisi ya ODPP kuharakisha mchakato wa kuandaa faili za mashtaka dhidi ya mteja wake ili kupata haki kwa mteja wake.



Kesi ya Mackenzi imekuwa ikijikokota kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, huku yeye na watuhumiwa wengine wakisalia korokoroni kipindi hicho chote.


“Mahakama iko tayari kuendelea, watuhumiwa wako tayari kuendelea, watetezi wako tayari lakini ODPP hayuko tayari. ODPP amekuwa na sababu nyingi, kutoka Mombasa alitoa sababu aliyoitaja kuwa uhaba wa waendesha mashtaka na katika mahakama hii amesema kwamba wanakabiliwa na changamoto za kifedha…” wakili Obonyo alisema.