MWINJILISTI mkongwe wa humu nchini, Reuben Kigame
amesifia hatua ya ujasiri ya mwanaharakati Okiya Omtatah ya kutangaza kuwa
atawania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Kupitia ukurasa wake wa X, Kigame alisema kwamba
Omtatah ni mmoja kati ya watu ambao amekuwa akifurahia kazi zao katika harakati
za kutafuta haki kortini na kwamba hatua yake ya kujitosa kwenye kinyang’anyiro
cha urais ni jambo la kushabikiwa.
“Heri
ya kuzaliwa Comrade @OkiyaOmtatah. Wewe ni pumzi ya hewa safi na Kenya
imebarikiwa kuwa na wewe hai kwa wakati huu. Wewe ni mshindani anayestahili
katika kinyang'anyiro cha urais ujao,” Kigame aliandika
akimtakia heri njema ya kuzaliwa mwanaharakati huyo.
Hata hivyo, Kigame aliweka hisia zake wazi kuhusu
hatua ya Omtatah kuwania urais, akimshauri kuungana naye ikiwa kweli ana nia ya
dhati ya kuirudisha Kenya katika kile alichokitaja kuwa ni ‘mkondo stahiki.’
Alimrai Omtatah kuiasa timu yake kutathmini uwezekano
wa kufanya kazi na timu yake ili kupata njia mwafaka ya kuikomboa nchi kutoka
utawala wa rais wa sasa William Ruto, ambao anahisi umewafeli Wakenya katika
ahadi nyingi za wakati wa kampeni.
“Natumai
timu yako ya tathmini ya rais itakuwa na unyenyekevu wa kuketi na timu yangu ya
rais ili kuunda mkakati mzuri wa kushirikiana. Usisahau kamwe, haikuhusu wewe
au Kigame, lakini njia bora zaidi ya kuokoa nchi yetu kutokana na uharibifu
zaidi, kurejesha maadili na kuweka viongozi wanaoongozwa na tabia, kumaliza wala
rushwa, na kupata maisha ya baadaye ya watoto wetu,”
Kigame alisema.
Alimaliza kwa kumtakia Omtatah maisha marefu na
kuishi hadi pale atakapotimiza ndoto yake ya kubadilisha Kenya kisiasa.
“Uishi
kuona siku nyingi zaidi za kuzaliwa na Mola akatujalia kuunda serikali ijayo
pamoja na wewe au Kigame kama rais ajaye.”
Kigame anamwandikia Omtatah ujumbe hii ikiwa pia naye
analenga kiti hicho cha urais.
Ikumbukwe Kigame alikuwa miongoni mwa wale waliotaka
kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2022 lakini hakufanikiwa kufika debeni
baada ya tume ya uchaguzi na mipaka, IEBC kumfungia nje kwa kutokuwa na
stakabadhi husika.
Kigame alihamia mahakamani kupinga hatua ya IEBC
kumtupa nje lakini kesi yake ilijikokota hadi baada ya kumalizika kwa uchaguzi
huo.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!