
MSHAURI wa masuala ya kiuchumi wa rais William Ruto,
Moses Kuria amewaasa wananchi kujiunga na mpango wa bima ya matiba ya SHA hata
kama hawampendi rais William Ruto.
Akizungumza katika eneobunge la Manyatta kaunti ya
Embu, Kuria aliwataka wananchi kufunguka macho na kutohadaiwa kwamba mpango wa
Taifa Care hauwafai.
Kwa mujibu wa Kuria, baadhi ya viongozi wanaowataka Wakenya
kutojisajili katika mpango wa SHA wana bima zao za nguvu za matibabu na
hawatokuwa nao hospitalini wakati watakuwa wanataabika kutafuta matibabu bila
bima ya SHA.
Akitolea mfano, Kuria alisema kwamba mwananchi wa
kawaida kuambiwa na kiongozi kutojisajili SHA ni sawa na kunywa sumu na
kutarajia Kuria afariki.

“Huu
mpango ni wako, si wa serikali, si wa Kuria wala rais Rut. Ni wako! Siku utagonjeka
ukiwa hospitalini utaanza kusema ni Ruto? Unajua mimi naona watu wengine
wakileta mchezo katika hili suala, ni kama kunywa sumu ukitarajia Moses Kuria
afe, na wewe ndiye umekunywa sumu. Nikakufaje na sumu ambayo wewe umekunywa?”
Kuria alihoji.
“Hivyo
wakati mtu anakuambia kutojisajili kwa Taifa Care, siku ya kugonjeka mktakuwa
na yeye kwenye wodi? Mtakuwa na yeye hospitalini? Wakati unafanya harambee ya
kupata pesa za matibabu sababu mtu wako amelazwa, mtakuwa na yeye? Kwa hivyo
tujichunge dhidi ya uongo jamani,” aliuliza zaidi.
Aliwataka wale wanaomchukia rais William Ruto
kutambua kwamba wanacheza karata tata na afya zao kwa kukataa kujisajili kwenye
SHA kisa hawampendi rais.
“Na
hata kama humtaki rais, si uingie katika hii SHA, ndio utibiwe, ndio uishi
miaka mingi ya kumtukana. Ukianza kumtukana na hujajisajili, utaishi miaka
mingi kweli ya kumtukana? Si angalau utibiwe ndio uweze kumtukana kesho jamani!
Kwa sababu huu mpango ni wako,” Kuria aliwaambia
wananchi.

Mshauri huyo wa rais alisema kwamba wengi
wanalalamika kuhusu mapungufu ya SHA bila kutambua kwamba ina miezi miwili tu
tangu izinduliwe.
Aliwataka Wakenya kuwa wenda pole katika kunyoosha
vidole vya lawama kwa mpango huo kwani ndio mwanzo uko katika hatua za mwanzo
mwanzo na kwamba utaboreshwa zaidi kadri siku zinazidi kusonga.
“Bado
zimesalia siku chache kabla ya SHA kuadhimisha miezi miwili. Sasa huyu mtoto wa
miezi 2 ndiye mnataka aanze kucheza raga jamani? Inawezekana kweli? Najua watu
wengi watakukatisha tamaa, lakini kadri wanavyokukatisha tamaa wakumbushe
kwamba ni miezi miwili tu, hata hatujaanza kufunga Kamba za viatu, na sasa ndio
tunaanza,” Kuria alitetea SHA.

Mpango wa SHA ulianza rasmi kufanya kazi mnamo Oktoba
mosi lakini umepokelewa na Wakenya kwa hisia vuguvugu, wengi wakionekana
kuukosoa mpango huo kwa kutokuwa sahihi katika matibabu yao.
Wiki jana katika hotuba yake kwa nchi katika kikao
cha pamoja cha mabunge yote mawili, rais Ruto aliutetea mpango huo akiwataka
wale wanaolalamika kuhusu mapungufu yake bila kujisajili kufanya hatua ya kujisajili
kwanza kabla ya kuanza kuibua maswali kuhusu matatizo ya SHA.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!