MWANAHARAKATI Morara Kebaso amemuomba Mungu kudhihirisha wazi uwepo wake katika azma yake ya kuwania urais wa Kenya katika uchaguzi mkuu ujao wa 2027.

Kupitia ukurasa wake wa X, Kebaso alimtaka Mungu kumuonyesha ishara kama kweli ni yeye anataka awanie urais, ili isije kuonekana kama ni mwenyewe anataka au pengine anafanya kazi ya bure.

“Bwana. Ikiwa ni wewe unayenituma, nipe ishara. Sitaki kufanya hivi kwa matamanio yangu au hamu yangu. Nionyeshe ishara ikiwa wewe ndiye unayenituma. Nataka kujua kama ni wewe unayezungumza name,” Kebaso alisema.

Ombi la Morara linajiri siku chache baada ya kutangaza rasmi kuwa atakuwa debeni katika uchaguzi wa urais mwaka 2027.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Mwanzilishi huyo wa chama cha INJECT alisema kuwa bila wasiwasi wowote, atakuwa miongoni mwa wale watakaomenyana na rais Ruto katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2027.

Hii ni licha ya kusutwa na wengi kwamba hana pesa za kumwezesha kufanikisha kampeni za urais ambazo humu nchini hushuhudia wagombea wakizunguka nchi nzima katika kipindi cha takribani miezi 4 ya kampeni.

Hata hivyo, Kebaso alikiri kwamba ni kweli yeye ni omba omba lakini akasema si kupenda kwake kuwa hivyo.

Mwanaharakati huyo alisema yeye, sawa tu na Wakenya wengine wengi, wameshrutishwa kuwa ombaomba na uongozi wa serikali ya rais Ruto ambayo anaituhumu kwa kufanya mazingira ya kiuchumi kuwa mabaya.

“Ndio sisi ni ombaomba. Lakini hatufurahii kuomba. Inashusha utu wetu. Ikiwa tungekuwa na pesa za kutosha, tungeendesha kampeni ya elimu ya uraia bila kuombaomba.”

“Vijana wengi nchini Kenya wamefanywa kuwa ombaomba kama sisi. Wanaomba kazi. Wanaomba kupandishwa vyeo. Wanaomba mtaji. Wanaomba chakula. Wanaomba takrima. Wanaomba jamaa zao. Wanaomba marafiki zao. Wanaomba wanasiasa. Ni wakati wa ombaomba kurudisha nchi yao. Kujitengenezea ajira na fursa. Kuwajengea wazazi nyumba na kuwalisha wadogo zao. Tunataka nchi yetu irudi,” Kebaso alisema katika tweet nyingine.

Licha ya kuweka wazi kwamba atakuwa debeni, mwanaharakati huyo alidokeza kuwa huenda akashirikiana na mwanaharakati mwenza, Okiya Omtatah katika kuendesha kampeni za kutwaa urais 2027.

Alisema hayo baada ya Omtatah naye kutangaza kuwa tayari ameanzisha mchakato mzima wa kutathmini hali itakayomuona akiwa debeni katika kinyang’anyiro cha urais 2027.