MWANAHARAKATI wa elimu ya kiraia, Morara Kebaso
amedokeza uwezekano wa kufanya kazi pamoja na mwanaharakati wa haki za
kibinadamu Okiya Omtatah kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Kupitia ukurasa wake wa X, Kebaso alifichua kwamba
amaheshimu sana seneta huyo wa Busia katika kile ambacho amefanya si tu katika
siasa za Kenya lakini pia katika kutafuta haki kiuharakati mahakamani.
Kebaso alisema kwamba huenda wakaungana pamoja katika
siku zijazo ili kutoa mwongozo mpya wa siasa za Kenya, na haswa katika uchaguzi
mkuu wa mwaka 2027.
“Okiya
Omtatah ni mtu mahiri mwenye hekima kubwa na uadilifu. Ndani yake naona maadili
ya pamoja. Niko tayari kufanya kazi naye siku moja katika siku zijazo,”
Morara Kebaso alisema.
Kauli ya Kebaso inajiri siku chache baada ya Omtatah
kudokeza kuwa huenda akajitosa kwenye kinyang’anyiro cha urais mwaka 2027.
Omtatah alisema kwamba tayari ameanzisha timu ya
kutathmini uwezekano na mazingira yote ambayo yatamwezesha kujitosa katika
uwanja huo mpana kumenyana na wanasiasa wengine wakongwe, akiwemo rais wa sasa,
William Ruto ambaye atalenga kutetea nafasi yake kwa muhula wa pili.
Akitangaza azma hilo mwishoni mwa juma lililopita,
Omtatah alifichua kuanzisha timu ya watu 6 ambao watafanya kazi kwa bidii za
mchwa kutathmini hakli nzima ya kumwezesha kuwania urais.
"Tuko katika wakati muhimu katika historia ya taifa letu, na wito
wa kuhudumu haujawahi kuwa wa dharura zaidi. Baada ya kutafakari kwa kina na
kushauriana na washauri wanaoaminika, viongozi wa jamii, na wananchi kutoka
tabaka mbalimbali, nina furaha kutangaza kuundwa kwa Kamati ya kutathmini Urais,”
alisema Omtatah Saturday.
Alisema kuundwa kwa timu hiyo ni "hatua muhimu katika
kuhakikisha kwamba maono yetu ya siku zijazo yanawiana na matumaini na
matarajio ya Wakenya."
Kamati hiyo itakayoongozwa na Mary Kathomi Riungu, itakuwa
ofisini kwa muda usiozidi miezi 18 na itavunjwa mara tu seneta huyo
atakapotangaza rasmi kuwania au uamuzi wake wa kutogombea.
Charles Ile Kabaiku atakuwa naibu mwenyekiti huku David John
Bwakali akiwa mwanamikakati wa kisiasa na mashinani.
Omatata ni seneta wa mara ya kwanza na mwanaharakati
anayejulikana kwa uhodari wake wa kuwasilisha kesi mahakamani kwa maslahi ya
umma, haswa dhidi ya sera za serikali anazoziona kuwa za uonevu na zisizo
halali. Alijiunga na siasa mnamo 2022 kama mgombeaji huru.
Tangazo hilo lilifuatia lile la Mwanaharakati Kebaso
aliyetangaza mwanzoni wa juma lililopita kwamba atakuwa debeni katika uchaguzi
wa urais 2027.
Kebaso alisema kwamba chama chake kipya cha INJECT kitatoa
wawaniaji wa nyadhifa mbalimbali kote nchini.
Wengine ambao wanatarajiwa kuwania urais ni pamoja na
Kalonzo Musyoka, Eugene Wamalwa, Jimmy Wanjigi miongoni mwa wengine.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!