GAVANA wa kaunti ya Trans Nzoia, George Natembeya amefichua kwamba kibarua chake kijacho ni kuwania urais wa Kenya.
Akizungumza katika ofisini yake, gavana huyo wa DAP-K
aliweka wazi kwamba pindi atakapokamilisha hatamu yake kama gavana wa Trans
Nzoia, ataelekeza macho na nguvu zote katika wadhifa wa urais.
Alichukua nafasi hiyo kuwashukuru watu wa Trans Nzoia
kwa kumpa nafasi kuwaongoza kama gavana wao, akisema kwamba baada ya hapo,
atajikita katika siasa za kitaifa.
Natembeya alisema kuwa hayuko tayari kuwania kama
naibu rais wa mwaniaji yeyote, katika kile anaelewa kuwa naibu rais hana usemi
mkubwa katika kupitisha baadhi ya sera.
“Kitu
chochote katika siasa kinawezekana. Lakini kutoka pahali ninapokaa, baada ya
kumalizana na hii kazi ambayo watu wa Trans Nzoia wamenipa, na ninashukuru kwa
kweli watu kwa kunipa heshima na upendeleo wa kuwahudumia, nitaenda kukita
macho yangu kwa ukakamavu kwenye urais,” Natembeya alisema.
“Pindi
nitakapomalizana na ugavana, sitaki kwenda kuwa naibu. Kwa sababu huwezi badilisha
vitu wakati wewe ni naibu. Nafasi yao ya kupenyeza huwa ni finyu, wakati
mwingine hata kupeana ushauri mdogo unaweza kupelekea kubanduliwa. Hivyo hatutaki
hivyo na Wakenya hafikiri wanataka mabadiliko kamili,”
aliongeza.
Kamishna huyo wa zamani wa mkoa wa Bonde la Ufa
alisema kwamba ili kuleta mabadiliko hayo ambayo watu wanataka, ni sharti
asimame kama rais na si naibu wa mtu yeyote.
Alitumia fursa hiyo kuzungumzia maazimio yake ambayo
angependa kuyaleta katika mabadiliko anayokusudia.
“Ninataka
kujenga nchi ambapo wakati unaona talanta unaikuza badala ya kuiua. Lakini hapa
Kenya kuna wanasiasa ambao baada ya kuona talanta, kitu cha kwanza kufanya ni
kuiua. Tunataka kuwa na nchi ambayo sisi wote tunajisikia kuwa sawa,”
alisema.
Gavana huyo alisema kwamba anashukuru sana kwa wale
ambao wanapendekeza yeye kusimama kama rais wa Kenya wakati mmoja.
Tamko lake linajiri siku chache baada ya watu kadhaa
kuweka wazi kuwa watawania urais katika uchaguzi wa 2027.
Wiki jana, wanaharakati Morara Kebaso na Okiya
Omtatah walitangaza kila mmoja kuwa watawania urais katika uchaguzi wa mwaka
2027.
Wawili hao watamenyana na rais William Ruto ambaye
atakuwa anatetea wadhifa wake kwa muhula wa pili lakini pia Eugene Wamalwa wa
DAP-K ambaye mapema mwezi Novemba alitangaza kupewa Baraka na chama hicho
kuwania urais.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!