Jamaa mrefu kutoka Kaunti ya Bungoma, Isaac Wekesa Otesa hivi majuzi alihudhuria kanisa la Salvation Healing Ministry la Mchungaji Victor Kanyari katika eneo la Kayole Junction, Nairobi.
Tukio la kushangaza lilitokea katika ibada ya siku ya Jumapili ambapo baba huyo wa watoto watatu aliyejizolea umaarufu baada ya maandamano ya Gen z alianguka wakati wa maombi.
Katika picha zilizofikia Radio Jambo, jamaa huyo mrefu alionekana akiombewa na Kanyari huku akiwa ameshikiliwa na mwanamume mwingine, kabla ya kuanguka na kujilaza kwenye madhabahu.
Baadaye alisaidiwa kuinuka kabla ya kupewa kipaza sauti ili kuzungumza na waumini.
“Tulipata fursa ya kumpokea Gen Z wa Bungoma kanisani na kila mtu alifurahia kutangamana naye. Mungu ambariki na afungue milango yake yote. AMINA!” Mchungaji Kanyari alisema katika taarifa yake.
Katika picha zingine, Bw Isaac Otesa alionekana akitangamana na waumini wengine wa kanisa hilo na kutoa hotuba mbele yao.
Isaac alipata umaarufu mkubwa miezi michache iliyopita baada ya kufananishwa na kijana Bradley Marongo almaarufu Gen z Goliath. Baadhi walidai kwamba wawili hao ni mandugu, na hilo liliibua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii.
Katika mahojiano ya mwezi Agosti, Isaac aliomba kukutana na kijana huyo aliyevuma wakati wa maandamano ambaye alidaiwa kuwa pacha wake.
Wakati huo, baba huyo wa watoto watatu alieleza jinsi alivyoshangaa baada ya kuona picha za Bradley zikivuma mitandaoni.
Isaac alieleza dhamira yake ya kujua kama kuna uhusiano wowote wa kindugu kati yake na Bradley, na hata akamkabili mama yake kwa maswali magumu.
“Mama, sasa vile huyo jamaa anasemekana yuko Nairobi, nami niko Bungoma, akisema niende mahali yuko ama yeye akuje Bungoma tuseme mimi ni ndugu yake, wewe utasema aje kama mzazi?” Isaac alimuuliza mama yake.
Bi Janet Wekesa ambaye alieleza waziwazi jinsi anavyojivunia mwanawe alibainisha kuwa yuko tayari kwa vipimo vyoyote kubaini iwapo wanaume hao wawili wana uhusiano wowote.
"Tutafuatilia, waende wapime kila kitu alafu tutajua," alisema.
Bi Janet hata hivyo alieleza imani yake kubwa kuhusu Isaac kuwa mwanawe wa kuzaa, akisema kwamba alimzaa nyumbani baada ya kukaa kwa miaka kadhaa kwenye ndoa bila mtoto.
“Yeye
kuzaliwa, niko na wenye walinizalisha, na sikuzalia hospitali. Nilizalia tu
nyumbani. Hata mimi mwenyewe sijawahi kufika huko Nairobi, sijawahi kwenda
huko,” alisema.
Pia aliondoa shaka kwamba babake Isaka alitoka nje ya ndoa na kupata mtoto mwingine.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!