Rais William Ruto ameagiza idara husika katika wizara za barabara na miundombinu na ile ya kawi kusitisha mara moja utoaji wa zabuni  kwa kampuni tata ya Adani.

Akizungumza wakati akitoa hotuba ya hali ya taifa kwa wananchi katika kikao cha pamoja cha wabunge na maseneta alasiri ya Alhamisi, Ruto aliagiza kusitishwa mara moja kwa michakato ya utoaji wa kandarasi kwa Adani.

Adani ilikuwa inalenga kupewa zabuni ya kusimamia uendeshaji wa uwanja wa ndege JKIA kwa miongo 3 pamoja pia na kampuni ya kusambaza umeme ya KETRACO.

“Sasa naelekeza katika kuendeleza misingi iliyoainishwa katika ibara ya 10 ya katiba ya uwazi na uwajibikaji na ya msingi kuhusu taarifa mpya zinazotolewa na vyombo vya uchunguzi na mataifa washirika, kwamba wakala wa ununuzi ndani ya wizara ya uchukuzi na wizara ya nishati na petroli mara moja kufuta mchakato unaoendelea wa ununuzi wa upanuzi wa JKIA,” rais Ruto alisema.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Ruto alisema kwamba agizo hili ni kutokana na habari ambazo serikali imepokea kutoka kwa mataifa marafiki kuhusu wasifu wa Adani.

Kiongozi wa taifa pia alitaka kuvunjwa mara moja kwa mkataba uliotiwa saini hivi majuzi kati ya kampuni ya kusambaza umeme ya KETRACO na Adani.

“Nimeagiza mara moja kufutwa kwa mchakato unaoendelea wa ununuzi wa upanuzi wa JKIA na pia mkataba uliokamilika hivi majuzi wa KETRACO,” alisema

Kughairiwa huko kulikuja baada ya ripoti kuashiria kuwa mmiliki wa Adani Group na wakurugenzi wake wameshtakiwa nchini Marekani kwa madai ya udanganyifu.

Msemaji wa Kundi la Adani hata hivyo alikanusha makosa yoyote kwa upande wa wakurugenzi na mmiliki akisema kushtakiwa haimaanishi kuwa wana hatia.