Mbunge wa Mumias ya Mashariki Peter Salasya ametangaza rasmi vita yake ya kuhakikisha anatokomeza ushawishi wa kinara wa chama cha ODM katika eneo la Magharibi mwa Kenya.

Kupitia video aliyorekodi, Salasya alisema kwamba tayari wameanza kutoa elimu ya kiraia kwa watu kuwaeleza jinsi watakavyoweza kusonga mbele kisiasa bila Raila Odinga katika eneo pana la Magharibi.

“Tumeshaanza kufanya zoezi la kutoa elimu ya kiraia, tukiwaambia watu wetu kutoka Magharibi mwa Kenya Raila Odinga ni nani,” Salasya alifichua.

Mbunge huyo kijana alidai kwamba Odinga tayari ameitisha kikao na wanachama wa Odinga katika kile alisema ni kuanza kuwatishia dhidi ya kutonena kwa sauti moja ya muongozo wa chama.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

“Na baada ya kusikia hivyo naambiwa ameita mkutano na wananchama akiwatishia kwa kutumia kamati za bunge. Ningependa kuwaambia watu kutoka Magharibi, wale waheshimiwa wanaoenda kumuona, ni kwamba tu kama hawawezi onyesha mshikamano watatolewa kwenye kamati za bunge,” Salasya alidai.

Mbunge huyo wa chama cha DAP-K alisisitiza kwamba msimamo wa watu kutoka Magharibi hautakuwa wa kupangwa bali watashawishika na ajenda na rekodi ya maendeleo.

Akionekana kuwalenga wale wanaomkosoa, Salasya alisema kuwa yeye ni Gen Z ambaye haogopi kitu chochote kando na kuoa tu.

“Mnanitishia mkinitusi mmesahau kwamba mimi ni Gen Z, kizazi changu sisi hatuogopi kitu chochote, tunachoogopa ni kuoa peke yake. Sasa mimi nataka niwaambie ya kwamba waite lakini sisi tunaanzisha mchakato wa kuenda kwa ground,” Salasya alisema.

Mbunge huyo alimtuhumu Odinga kwa kile alisema ni kuitetea kampuni ya Adani ambayo inalenga kuchukua kandarasi ya kuendesha uwanja wa ndege wa JKIA kwa miongo mitatu.

Salasya pia alidai kwamba Odinga analenga kusukuma kuondolewa kwa hela za ustawishaji wa maeneo bunge, CDF na kupelekwa chini ya usimamizi wa magavana.

“Eti unataka CDF na KeRRA itolewe kwa kiwango cha maeneo bunge na ipelekwe chini ya usimamizi wa magavana, eti halafu nikuunge mkono, mimi ni mwendawazimu?” Salasya aliuliza.