Utafiti mpya umebaini jinsi wafanyibiashara wa pombe wanawashawishi vijana kujitosa katika unywaji kwa kubuni majina ya kuvutia ya aina za pombe mbalimbali.

Ripoti hiyo iliyotolewa na Shule ya Sayansi ya Afya ya Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda, imefichua jinsi ushawishi wa majina ya chapa za pombe yanavutia kwa vijana.

Hii ni licha ya serikali mbalimbali haswa ukanda wa Afrika Mashariki kuzidisha vita dhidi ya pombe haramu za kuuzwa mitaani kwa njia za kimagendo.

Licha ya kuondolewa kwa mifuko ya pombe maarufu kama sachet sokoni, ripoti hiyo inaangazia kuhama kwa chupa ndogo, ambazo sasa zinauzwa kwa wanywaji wa umri mdogo, haswa nchini Uganda.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Kulingana na utafiti wa miaka miwili uliofanywa kati ya Juni 2022 na Novemba 2024 katika wilaya za Gulu na Wakiso, chupa ndogo, kwa kawaida 200ml au chini ya hapo, zinauzwa kwa bei ya chini sana.

Inashangaza kwamba bidhaa hizi zinatengenezwa na makampuni ambayo hayajasajiliwa yanayofanya kazi kinyume cha sheria, hasa vijijini.

Profesa Nazarius Mbona Tumwesigye kutoka Shule ya Afya ya Umma ya Chuo Kikuu cha Makerere alisisitiza kwamba kuenea kwa unywaji pombe kumezidisha mzigo katika mfumo wa afya watu wengi barani Afrika.

Utafiti huo uliangazia kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza yanayohusishwa na unywaji pombe, na kuweka mkazo zaidi kwenye rasilimali za afya ya umma.

"Mwelekeo unaokua wa matumizi mabaya ya pombe ni janga la afya ya umma, na kuchangia kwa kiasi kikubwa kuenea kwa magonjwa yanayohusiana na pombe," alisema Prof Tumwesigye.

Uganda inashika nafasi ya kwanza barani Afrika kwa matumizi ya pombe kwa kila mtu, na wastani wa lita 12.21 zinazotumiwa kila mwaka kwa kila mtu.