Mwanafunzi mmoja wa chuo kikuu mnamo siku ya Jumatatu alishtakiwa katika Mahakama ya Milimani kwa madai ya kuchapisha habari za uwongo kuhusu rais William Ruto kwenye mitandao ya kijamii.

Mwanafunzi huyo anayesemekana kujitambulisha kwa jina la ‘Landlord @bozgabi’ kwenye mtandao wa X anaripotiwa kuchapisha picha ya msafara wa mazishi ukiwa na jeneza lililofunikwa kwa bendera ya Kenya, na kusindikizwa na maafisa wa kijeshi wakiwa wamevalia sare zao za sherehe.

Katika maelezo ya posti yake, mshtakiwa anasemekana aliandika maelezo yanayopendekeza kuwa ni mwili wa Rais William Ruto ulikuwa ukisafirishwa.

Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP), katika taarifa ilisema kuwa mshtakiwa aliifanyia ukarabati tarehe ili kufanya posti yake ionekane kuwa halisi.

"Kosa hilo linasemekana kutendeka mnamo Novemba 13, 2024, katika eneo lisilojulikana ndani ya Jamhuri ya Kenya," ripoti ya ODPP ilisomeka.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Mshtakiwa alikana mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi Benmark Ekhumbi.

Alipewa bondi ya KSh 100,000 na dhamana mbadala ya pesa taslimu KSh 50,000.

Kesi hiyo imepangwa kutajwa tena Desemba 4, 2024.