Taarifa ya maaskofu wa kanisa la katoliki nchini siku ya Alhamisi imeonekana kutonesha kidonda cha serikali baada ya wakuu wa idara mbali mbali za serikali kujitokeza kujibu madai ya maaskofu hao.
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Elimu na Inspekta Jenerali wa Polisi imekashifu kauli ya Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Kenya na kusema kuwa ni potofu na inapotosha umma. Taarifa zilizotolewa na waziri wa Afya, Deborah Mulongo, mwenzake wa Elimu, Migos Ogamba na IG Douglas Kanja zimewalaumu maaskofu kwa kufumbia mamcho maendeleo makubwa yaliyofikiwa na serikali kuhusu masuala yanayohusiana na Mamlaka ya Afya ya Jamii, ufadhili wa elimu ya vyuo vikuu, mtaala wa CBC na uchunguzi wa mauaji na utekaji nyara wa watu kinyume cha sheria nchini.
CS Deborah alipuuzilia mbali madai ya maaskofu hao kuwa serikali imekataa kulipa madeni ambayo hospitali za kidini zinadai Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF). Alikariri ahadi ya serikali kulipa madeni yote ya NHIF kupitia SHA. Dkt Barasa alibainisha kuwa kufikia sasa, shilingi bilioni 7.58 zilikuwa zimetengwa kulipa deni alilosema kwa sasa ni shilingi bilioni 19.
"Kufikia tarehe 4 Oktoba 2024, NHIF iliyofungwa ilikuwa na deni la Ksh.19B kwa watoa huduma mbalimbali wa afya, madeni yaliongezeka kwa muda wa zaidi ya miaka 10."
Waziri wa Elimu Migos Ogamba kwa upande wake alikashifu maaskofu hao huku akitetea utekelezwaji wa Mtaala wa CBC tangu kuanzishwa kwake 2017 na mtindo mpya wa Ufadhili wa Vyuo Vikuu, akitaja ufanisi katika programu zote mbili. Kulingana na Ogamba, Kanisa lilikosea katika maelezo yake ya programu hizo mbili kama ‘kuporomoka’ kwa vile serikali ilikuwa tayari imefanya hatua makubwa katika utekelezaji wa programu zote mbili kwa kuwekeza pakubwa.
“Ubora wa CBC na muundo wake umekuwa chini ya mashauriano ya kina ya wadau na ushirikishwaji wa umma. Haya yalijumuisha Kongamano la Maaskofu wa Kikatoliki nchini Kenya, walioshiriki katika kazi ya Chama cha Rais kuhusu Marekebisho ya Elimu.”
IG Kanja alilaumu Kanisa kwa kutozingatia kazi ya idara ya usalama kuhusu utekaji nyara, utesaji, mauaji, na kuongezeka kwa mauaji ya wanawake nchini. IG alisisitiza kuwepo kwa uchunguzi, akiorodhesha kuwa idara ya polisi imewatia mbaroni watu 1552 nchini kote kuhusiana na matukio hayo na kuunda Kitengo maalum kuchunguza visa vya watu kutekwa nyara na idara maalum ya Jinsia kushughulikia kuongezeka kwa utekaji nyara na mauaji ya wanawake mtawalia.
“NPS ilirekodi majeruhi 495 kwa maafisa wa polisi, majeruhi 347 kwa raia, vifo vya raia 42, na visa 69 vya uharibifu mkubwa wa magari ya serikali. Aidha, kulikuwa na kesi 57 zilizoripotiwa za watu waliopotea, ambapo 22 walipatikana wakiwa hai, 6 walikutwa wamekufa huku 29 wakiwa bado hawajulikani waliko na juhudi zinaendelea kuwatafuta. Wakati wa maandamano, NPS ilikamata watu 1552 kote nchini,” Kanja alisema.
Kiongozi wa Wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot pia alijibu taarifa ya makasisi hao.
"Ni jambo la kusikitisha kwamba viongozi wa kidini wanageukia mambo ya jumla. Ikiwa wana hoja na kiongozi mmoja mmoja, watafute suluhu kupitia vyombo husika vya kikatiba badala ya kulaani bunge zima," Cheruiyot alisema.
Kanisa Katoliki siku ya Jumatano lilishutumu utawala wa Rais William Ruto kutokana na mauaji yasiyoeleweka, utekaji nyara, ufisadi ulioenea na udanganyifu unaoongezeka.
Katika taarifa yao maaskofu hao kupitia Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya (KCCB), waliikosoa serikali kwa kuendeleza mazingira ambayo wananchi wamezoea uongo unaoenezwa na wanasiasa.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!