Tony Sherman na Kendi, vijana wa Gen Z waliogonga vichwa vya habari za burudani humu nchini miezi 3 iliyopita baada ya kudai kukutana kwenye mandamano na safari ya penzi lao kung’oa nanga, wameachana.

Akithibitisha habari hizo za kuvunja moyo kupitia ukurasa wake wa Instagram, Sherman alifichua kwamba ndoa yao haipo hai tena kwani kila mmoja ameamua kuchukua mkondo wake wa maisha kivyake.

Sherman na Kendi walikutana kwenye maandamano ya kupinga utawala wa rais Ruto mnamo mwezi Juni na kupendana papo hapo.

Wiki kadhaa baadae, wawili hao walifunga harusi mwishoni mwa Agosti, hafla ambayo ilifanyika katikati mwa jiji la Nairobi na kushuhudiwa na mamia ya wana jiji.

Hata hivyo, takribani miezi miwili baadae, wawili hao wameshindwa kuendelea na uhusiano wao katika kile ambacho Sherman alisema kuwa mambo yametokea mengi katika kipindi hicho kifupi cha ndoa yao.

“Hakuna tena maandamano couple. Kuna mwenye atasema ilikua brief kama maombi ya chakula. Nataka kutangaza rasmi kuwa sijaoa tena. Mambo yamekuwa mob, maandamano yamekuwa mingi!” Tony Sherman alitangaza.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Kijana huyo alitangaza kwamba hajafa moyo katika harakati za kutafuta mpenzi wa kudumu naye.

Alisema kwamba kwa sasa yuko mawindoni kumtafuta mrembo atakayechukua nafasi ya Kendi katika moyo wake, akisema kwamba kigezo cha pekee ambacho atakizingatia ni kwamba mrembo huyo asiwe mtumizi wa bangi.

“Moyo wangu uko wazi kwa msichana yeyote pale bora tu usiwe unavuta bangi. DM, CV muhimu...” aliongeza.

Kuachana kwao kunajiri licha ya kwamba Sherman aliwatoa watu wasiwasi kuhusu upendo wao wakati wa mahojiano na Kioko Nicolas mwezi Julai.

“Hatuchezi michezo. Nilipendezwa kwake hapa," alihakikishia, akimkumbatia.

Hata hivyo, kuna baadhi walihisi kwamba wawili hao wanafukuzia kiki, wengine hata wakidai kwamba huenda hakukuwa na penzi kati yao kama walivyodai, wakisema huenda ni mchongo walisuka ili kupata umaarufu kwenye mitandao ya kijamii.