Marekani imeipongeza Kenya kwa kuchukua msimamo thabiti dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya baada ya kuteketeza zaidi ya kilo 1,000 za dawa aina ya 'methamphetamine' zenye thamani ya Shilingi bilioni 8.2. Ubalozi wa Marekani nchini Kenya ulisema kuwa hatua ya kuteketeza dawa hizo jijini Mombasa ni hatua muhimu katika kuondoa dawa haramu kwenye soko la Afrika Mashariki. Ubalozi huo pia ulisifu ushirikiano wake wa muda mrefu na Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya cha DCI, kupitia mafunzo ya pamoja na kubadilishana taarifa ili kukabiliana na biashara haramu ya dawa za kulevya.