Kamati ya Bunge ya Elimu itahitimisha awamu ya kwanza ya ushirikishwaji wa umma kuhusu Miswada sita ya mageuzi ya elimu hii leo, kwa kufanya kikao cha kusikiliza maoni jijini Nairobi. Kikao hicho kitafanyika katika majengo ya Bunge kuanzia saa nne asubuhi hadi saa kumi na moja na nusu jioni, na hivyo kuhitimisha mzunguko wa awali wa kamati hiyo wa kukutana na wananchi katika kaunti 31. Kamati hiyo imewaalika wakaazi wa Nairobi na wadau wa elimu kuhudhuria kongamano hilo na kuwasilisha maoni, hoja na mapendekezo yao kuhusu mageuzi hayo yanayopendekezwa.