Usalama umeimarishwa katika kiwanda cha Bamburi huko Kisauni, Mombasa, kabla ya zoezi la kuteketeza dawa za kulevya aina ya 'methamphetamine' zenye thamani ya Shilingi bilioni 8.2. Maafisa wakuu wa usalama wanatarajiwa kusimamia zoezi hilo, wakiongozwa na Waziri wa Usalama, Kipchumba Murkomen. Dawa hizo za kulevya zilinaswa kutoka kwenye meli iliyozuiwa katika Bahari ya Hindi mwezi Oktoba mwaka uliopita. Shehena hiyo inahusishwa na kesi inayoendelea katika Mahakama ya Shanzu, ambapo washukiwa sita wanakabiliwa na mashtaka ya kusafirisha zaidi ya kilo elfu moja za 'methamphetamine'.