Maafisa wa polisi na wale wa mashirika mbalimbali ya serikali wamefanya msako katika eneo linaloshukiwa kuwa kichinjio haramu cha punda katika Wadi ya Kalimoni, Juja, Kaunti ya Kiambu, kufuatia ripoti za mizoga ya punda kutupwa eneo hilo. Maafisa hao walikuta punda 30 walio hai na katika hali mbaya ndani ya jengo la ghorofa mbili, lakini hakuna washukiwa waliokuwepo. Pia walipata visu na, mabaki ya kichinjio, mifuko ya plastiki na vifaa vya kufungashia vilivyoshukiwa kutumika kwa ajili ya nyama ya punda. Jirani mmoja aliwaambia polisi kuwa shughuli za kuchinja zilikuwa zikisikika mara kwa mara nyakati za usiku, takriban mara moja kwa wiki.