Tume ya Uwiano na Utangamano NCIC imemwita Mbunge wa Kimilili, Didmus Barasa, na Mbunge wa Turkana Kusini, John Ariko, kufuatia kauli walizotoa hadharani katika kaunti za Bungoma na Turkana. Barasa anachunguzwa kuhusiana na matamshi yake kuhusu uteuzi wa watu kutoka eneo lililokuwa mkoa wa magharibi, kushika nyadhifa za juu serikalini, pamoja na jinsi wagombea kutoka jamii mbalimbali walivyoshughulikiwa wakati wa mahojiano. Kwa upande mwingine, Ariko aliitwa kujibu maswali kuhusu uhusiano kati ya jamii za Turkana na Pokot, usalama, wizi wa mifugo, na ugavi wa mapato yatokanayo na eneo la mafuta la Lokichar.