Maafisa wa upelelezi wanachunguza tukio ambapo mwanamke mwenye umri wa miaka 23 alijeruhiwa kwa risasi wakati wa wizi wa mabavu huko Maweni, Kisauni, Kaunti ya Mombasa, baada ya kundi la wanaume watatu wenye silaha kukabiliana na maafisa wa polisi waliokuwa wakijibu ripoti za mashambulizi dhidi ya wananchi. Tukio hilo lilitokea mwendo wa saa tisa alfajiri  Jumamosi, katika eneo la Hodi Hodi. Kulingana na polisi, maafisa waliokuwa doria walipokea taarifa kwamba kundi la watu wanaoshukiwa kuwa majambazi, wakiwa na mapanga, lilikuwa likiwatisha na kuwahangaisha wakaazi wa eneo hilo.