Mamlaka katika Kaunti Ndogo ya Sabatia zimeibua wasiwasi kuhusu ongezeko la visa vya unajisi na unyanyasaji wa kingono, zikiwataka wadau kuimarisha juhudi za kuwalinda watoto na kuhakikisha wahalifu wanakabiliana na sheria. Kamishna Msaidizi wa Kaunti ya Sabatia, Martin Kagucia aliwaonya wakaazi dhidi ya kushughulikia kesi za unajisi kwa njia zisizo rasmi au kinyume cha sheria. Kagucia alionya kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watu wanaojaribu kuwalinda wahalifu au kutatua kesi hizo nje ya mfumo wa kisheria uliowekwa.