Picha hii, iliyopigwa Septemba 24, 2025, inaonyesha mabango ya mkutano wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia-Pasifiki (APEC) mjini Gyeongju, Korea Kusini. (Picha na Jun Hyosang/Xinhua)
Watu kutoka matabaka yote nchini Korea Kusini wanatazamia kwa hamu ziara ijayo ya Rais wa China Xi Jinping kuanzia Oktoba 30 hadi Novemba 1.
Rais wa China Xi Jinping atahudhuria Mkutano wa 32 wa Viongozi wa Kiuchumi wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia-Pasifiki (APEC) mjini Gyeongju na kufanya ziara ya kiserikali nchini Korea Kusini kuanzia Oktoba 30 hadi Novemba 1 kwa mwaliko wa Rais wa Korea Kusini Lee Jae-myung.
Watu kutoka matabaka yote nchini Korea Kusini wanatazamia kwa hamu ziara hiyo. Wana imani kuwa safari hiyo itaongeza uaminifu wa kisiasa wa pande mbili, kuimarisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara, kuwezesha urafiki kati ya watu, na kuelekeza ushirikiano wa kimkakati kati ya China na Korea Kusini katika kiwango cha juu zaidi, na kuleta manufaa zaidi kwa watu wa nchi hizo mbili.
SAFARI MPYA
Baada ya miaka 11, Xi anatarajiwa kuitembelea tena Korea Kusini.
“Ziara hiyo itakuwa kichocheo muhimu cha kuimarisha zaidi uhusiano wa ujirani mwema na urafiki wa pande mbili. Inatarajiwa kuwa viongozi wa nchi hizo mbili wataongeza uaminifu wa pamoja, kujenga makubaliano, kuchochea ushirikiano na mawasiliano yenye nguvu zaidi katika biashara, uchumi na mahusiano ya kitamaduni, na kutoa msukumo mpya kwa amani na maendeleo ya kikanda,” alisema Yoon Hu-duk, mbunge wa Bunge la Taifa la Korea Kusini.
Wakati wa ziara yake ya kiserikali nchini Korea Kusini mwezi Julai 2014, Xi alitoa hotuba katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Seoul, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha urafiki na ushirikiano wa pande mbili.
Akiwa amevutiwa na hotuba hiyo, Woo Su-keun, mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Asia ya Mashariki ya Korea, alisema: “Ziara hiyo ilikuwa hatua ya kihistoria katika maendeleo ya uhusiano kati ya Korea Kusini na China.”
“Ninatazamia kusikia mipango mipya ya Xi kwa maendeleo ya uhusiano kati ya China na Korea Kusini,” alisema Woo, ambaye kwa muda mrefu amekuwa akifuatilia uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia mwaka 1992, nchi hizo mbili zimevuka tofauti za itikadi na mifumo ya kijamii, na kuendeleza kwa bidii mawasiliano na ushirikiano katika nyanja mbalimbali, zikichangia mafanikio ya kila mmoja na maendeleo ya pamoja.
Mwezi Juni, Xi alifanya mazungumzo ya simu na Lee, akisema kuwa China na Korea Kusini zinapaswa kushikilia dhamira ya awali ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia, kudumisha ujirani mwema na urafiki, kujitahidi kufikia manufaa ya pande zote na matokeo ya kushinda pamoja, na kuinua ushirikiano wao wa kimkakati hadi kiwango cha juu zaidi.
Akikumbuka mikutano yake kadhaa na Xi, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon aliiambia Xinhua kuwa ziara ijayo ya Xi nchini Korea Kusini ni ishara thabiti ya kuimarisha zaidi uhusiano kati ya China na Korea Kusini, akiongeza kuwa kama majirani muhimu, China na Korea Kusini zinabeba wajibu wa pamoja katika kudumisha uthabiti wa minyororo ya ugavi ya kikanda na kukuza ujumuishaji wa kikanda.
Ban Ki-moon, mwenyekiti wa Jukwaa la Boao kwa Asia na aliyekuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, akizungumza katika mahojiano na Xinhua mjini Seoul, Korea Kusini, Oktoba 1, 2025. (Xinhua/Yao Qilin)
Ban, ambaye pia aliwahi kuwa waziri wa mambo ya nje wa Korea Kusini, alitarajia kuwa nchi hizo mbili zitachukua diplomasia ya viongozi wa nchi kama mwanzo mpya, kubadilisha urafiki kati ya Korea Kusini na China kuwa matokeo ya vitendo, na kutoa mchango mkubwa zaidi kwa amani na ustawi wa kikanda.
Hwang Jae-ho, mkurugenzi wa Taasisi ya Mkakati wa Dunia na Ushirikiano, alisema kuwa misingi ya “urafiki, uaminifu, manufaa ya pamoja na ujumuishi” inayosimamia diplomasia ya ujirani ya China imeweka mwelekeo wazi wa ushirikiano wa kikanda.
“Chini ya uongozi wa diplomasia ya viongozi wa nchi, China na Korea Kusini zinaweza, kwa misingi ya heshima ya pande zote na manufaa ya pamoja, kuvuka tofauti za mifumo na kufungua ukurasa mpya wa maendeleo ya pamoja,” alisema Hwang.
USHIRIKIANO WA KUSHINDA PAMOJA
Katika Bandari ya Incheon nchini Korea Kusini, makontena yenye nembo za makampuni makubwa ya usafirishaji ya China yanapakiwa na kupakuliwa na kreni za kiotomatiki kabla ya kuelekezwa kwenye maeneo mbalimbali duniani.
Hii ni mojawapo ya njia zenye shughuli nyingi zaidi za kubadilishana biashara na uchumi kati ya China na Korea Kusini. “Kwa sasa, kiasi cha biashara ya makontena ya bandari yetu na China kinachangia asilimia 60 ya jumla ya biashara ya Bandari ya Incheon,” alisema Nam Sang-ki, meneja mkuu wa Sun Kwang Newport Container Terminal Co., Ltd.
Ziara ijayo ya Xi “itaingiza uhai mpya” katika nyanja kama vile lojistiki ya bandari na utengenezaji wa vifaa, na kuendeleza zaidi ushirikiano katika ujenzi wa bandari mahiri na za kijani, aliongeza Nam.
Watu watembelea banda la Korea Kusini wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya China ya Biashara ya Huduma (CIFTIS) ya mwaka 2023 katika Kituo cha Kitaifa cha Mikutano cha China mjini Beijing, mji mkuu wa China, Septemba 4, 2023. (Xinhua/Ren Chao)
Kwa kuwa minyororo yao ya uzalishaji na ugavi imeunganishwa kwa kina, China imekuwa mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa Korea Kusini kwa miaka 21 mfululizo, huku Korea Kusini ikiwa mshirika wa pili kwa ukubwa wa kibiashara wa China.
Yoon Do-son, Mkurugenzi Mtendaji wa CJ China, alisema ziara ijayo itaunda mazingira chanya ya kisiasa na kuongeza imani miongoni mwa wafanyabiashara.
“Kama kampuni ya Korea Kusini yenye dhamira ya muda mrefu nchini China, tunaamini kuwa mazingira mazuri yanayochochewa na diplomasia ya viongozi wa nchi yatanufaisha juhudi zetu za kujikita nchini humo na ushirikiano wa kushinda pamoja na washirika wa China,” alisema Yoon. “Daima tumekuwa na imani kubwa katika mustakabali wa uhusiano wa kiuchumi na kibiashara wa pande mbili.”
Makubaliano ya Biashara Huria kati ya China na Korea Kusini yalianza kutekelezwa mwaka 2015. Tangu wakati huo, kiwango cha biashara huria na uwekezaji wa pande mbili kimeendelea kuongezeka, huku ushirikiano ukipanuka kutoka viwanda vya jadi hadi nyanja zinazoibukia kama utengenezaji wa hali ya juu, biashara ya mtandaoni ya mipakani na uchumi wa kidijitali.
Park Soong-chan, mwenyekiti wa Chama cha Korea-China na profesa wa Chuo Kikuu cha Yong In, alisema ziara ya Xi inatarajiwa kuchochea ushirikiano mpana na wa kina zaidi.
Korea Kusini na China zinaweza kuchunguza sekta zaidi zenye kukamilishana na kutekeleza ushirikiano unaolenga siku zijazo, kwa kuwa kila upande una nguvu zake katika viwanda vya kijani, teknolojia ya kibaolojia na nyanja nyingine, alisema profesa huyo.
Leo, visafisha sakafu vya roboti vya China vinapendwa na familia nyingi za Korea Kusini, huku roboti za utoaji huduma zikiwa tayari zinafanya kazi katika migahawa na hoteli mjini Seoul. Kuongezeka kwa uwepo wa ubunifu wa China katika soko la Korea Kusini kunaashiria mtazamo mpya wa ushirikiano na mwingiliano wa viwanda kati ya nchi hizo mbili.
Jeon Byung-seo, mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Fedha na Uchumi wa China, alisema hili linatumika kama nguvu ya kusukuma mbele uboreshaji wa viwanda nchini Korea Kusini.
China na Korea Kusini zina uwezo mkubwa wa kushirikiana katika nyanja zinazoibukia kama uchumi wa kidijitali na akili bandia, alisema mtaalamu huyo, akibainisha kuwa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili utaongeza ushindani wao katika soko la dunia.
Lee Hee-sup, katibu mkuu wa Sekretarieti ya Ushirikiano wa Pande Tatu, aliiambia Xinhua kuwa China inaweka mkazo katika kuendeleza nguvu mpya za uzalishaji wa ubora wa juu, jambo litakaleta fursa mpya kwa uchumi wa dunia, akiongeza kuwa ziara ya Xi haitakuza tu zaidi maendeleo ya uhusiano wa kiuchumi na kibiashara wa pande mbili, bali pia itaingiza imani na uhai mpya katika ushirikiano wa kiuchumi katika eneo lote la Asia-Pasifiki.
URAFIKI ULIOJENGEKA KWA MUDA MREFU
Viongozi wa nchi zote mbili walisisitiza katika mazungumzo yao ya simu mwezi Juni kwamba pande zote zinapaswa kuimarisha mawasiliano ya watu kwa watu na ya kitamaduni ili kuongeza uelewano wa pamoja na kuimarisha uungwaji mkono wa umma, na hivyo kupanda mbegu za urafiki kati ya China na Korea Kusini ndani ya mioyo ya watu wa nchi hizo mbili.
Safari huru kwenda China zimeongezeka kwa kasi baada ya China kutekeleza sera ya majaribio ya kuingia bila visa kwa raia wa Korea Kusini mwezi Novemba uliopita.
Kuanzia taa za neon za Bund mjini Shanghai hadi askari wa Terracotta mjini Xi’an, Wakorea Kusini wengi zaidi wanachunguza China na kuhisi joto la urafiki wa pande mbili.
“Matunzo makini ya China kwa maeneo ya kihistoria yanayohusiana na Korea Kusini huko Shanghai, Chongqing, Hangzhou, Nanjing na maeneo mengine yanaonyesha heshima kwa historia na pia yanafanya watu wa Korea Kusini wahisi kwa kina urafiki kutoka China,” alisema Nam Jin, naibu mkurugenzi mkuu wa masuala ya Asia ya Kaskazini Mashariki na Asia ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kusini.
“Mawasiliano ya watu kwa watu yanatoa nafasi zaidi ya uelewano na huruma,” alisema Lee Jeung-eun, rais wa Klabu ya Daraja la Kichina mjini Seoul, akieleza matumaini kuwa ziara ya Xi itaongeza urafiki na imani kati ya watu wa nchi hizo mbili na kuwa kichocheo cha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi, na kuielekeza uhusiano wa pande mbili katika mwelekeo chanya zaidi.
Mawasiliano kati ya watu ndiyo kifungo cha ndani kabisa kinachodumisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili, alisema Lee Wook-yeon, mkuu wa Chuo cha Sayansi ya Binadamu katika Chuo Kikuu cha Sogang.
Akibainisha kuwa China na Korea Kusini zote zinaweza kuelewa falsafa ya Confucius na kuzungumzia Li Bai — mshairi mkubwa wa Enzi ya Tang ya China — kwa pamoja, Lee alisema: “Aina hii ya muunganiko wa kiroho ndiyo nguvu ya kudumu zaidi.”
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!