
Kwenye eneo la ujenzi wa Mradi wa Maji wa Quilonga unaotekelezwa na Shirika la Ujenzi wa Umeme la China (PowerChina) mashariki mwa Luanda, mji mkuu wa Angola, wafanyakazi wanaendelea na majukumu yao kwa mpangilio mzuri.
Figueira Kalunga, fundi anayesimamia usalama, huzunguka eneo la ujenzi akikagua kwa makini kofia, mikanda ya usalama na vifaa vingine vya kujikinga vinavyotumiwa na wafanyakazi.
Kalunga amehusika katika miradi kadhaa ya PowerChina tangu mwaka 2017, akiianza kazi yake kama fundi chuma.
“Ninajivunia kuwa sehemu ya mradi huu unaoboresha maisha ya watu. Hauleti tu ajira kwa Wamangola wengi, bali pia utanufaisha idadi kubwa ya wakazi mara utakapo kamilika,” alisema.
Kwa muda mrefu, Luanda imekuwa ikikabiliwa na uhaba mkubwa wa maji kutokana na ukame, miundombinu ya zamani na uwezo mdogo wa kusafisha na kusambaza maji.
Antonio Fernandes Rodrigues Belsa da Costa, katibu wa serikali anayehusika na maji katika Wizara ya Nishati na Maji ya Angola, alisema katika eneo la mradi kwamba mji mkuu bado una upungufu wa maji wa hadi asilimia 50, huku baadhi ya maeneo yakipata maji mara moja tu kila baada ya siku mbili au tatu.
Kwa mujibu wa meneja wa mradi Zhang Qiang, Mradi wa Maji wa Quilonga unahusisha kituo cha kusukuma maji ghafi chenye uwezo wa lita 570,000 za ujazo kwa siku, bomba la kusafirisha maji ghafi lenye urefu wa kilomita 12.5, kiwanda cha kusafisha maji chenye uwezo wa lita 500,000 za ujazo kwa siku, pamoja na vituo vitano vya usambazaji.
Ujenzi unaendelea kulingana na ratiba, na mara utakapo kamilika, mradi huu utapunguza kwa kiwango kikubwa uhaba sugu wa maji mashariki mwa Luanda, alisema Zhang.

Zhang Peng, mhandisi mkuu, alisema kituo cha kusukuma maji kilichoko kwenye kingo za Mto Kwanza kilikumbana na changamoto nyingi za ujenzi kutokana na ardhi yenye unyevunyevu na msingi unaohitaji kuchimbwa kwa kina.
“Kwa kutumia mbinu bunifu za uhandisi, tumeweza kuweka msingi imara kwa ajili ya muundo mkuu,” alisema.
Zaidi ya ujenzi, timu ya mradi imejitahidi kupunguza tofauti za kanuni na viwango vya kiufundi kati ya China na Angola.
Pia wamesaidia kukuza maelewano ya kitamaduni kwa kuandaa shughuli mbalimbali, kutoa mafunzo ya lugha, na kuajiri wahandisi wa kienyeji waliopata masomo nchini China, hatua ambayo inasaidia kuongeza ushirikiano na uelewa kati ya wafanyakazi.
Helmano Adriano, msimamizi wa manispaa ya Bom Jesus ambako mradi huu unatekelezwa, alisifu kujitolea kwa PowerChina kusaidia jamii kupitia miradi ya kijamii kama vile ujenzi wa mifumo ya maji ya kunywa, usakinishaji wa mtandao wa umeme, na kusaidia mipango ya kijamii ambayo inanufaisha moja kwa moja maelfu ya wakazi.
“Mradi wa Maji wa Quilonga utaimarisha kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa maji jijini na kimsingi kufunga pengo lililopo. Tunaamini kwamba ifikapo mwaka 2026, mara utakapokamilika, utapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la upungufu wa maji Luanda,” alisema Belsa da Costa.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!