Diana Marua na mwanawe Morgan Bahati//INSTAGRAM

YOUTUBER Diana Marua amemshauri mwanawe wa kiasili Morgan Bahati kutokuwa na hulka ya kuchumbiana na wapenzi wengi kwa wakati mmoja kama ambavyo yeye alifanya katika maisha yake ya ujana.

Kupitia kipindi chake cha maswali na majibu na Morgan kwenye chaneli yake ya YouTube, Diana Marua alimtaka Morgan kumuuliza swali lolote na angeweza kumpa jibu kwa ufasaha.

Morgan alitaka kujua ni jambo lipi baya ambalo Diana alifanya katika maisha yake ya ujana na ambalo asingependa yeye [Morgan] kulifanya.

Bila woga, Diana alisimulia kwa majuto jinsi alijiingiza katika harakati za kuingia katika mahusiano ya mapenzi na wanaume kadhaa kwa wakati mmoja, akisema ni jambo ambalo asingependa limtokee Morgan.

“Kuna vitu vingi ambavyo nilivifanya kama tineja na ambavyo sijivunii kusema ukweli. Jambo la kwanza katika umri wangu wa ujana nilichumbiana na watu wengi. Kwa ufupi ni kwamba sikuwa muaminifu kwa mpenzi mmoja,” Diana alifungua jungu kuu la siri.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Diana Marua na mwanawe Morgan Bahati//INSTAGRAM

Kulingana naye, hulka hii ya kuwa na wapenzi wengi kwa mpigo ili mpotezea bahati yake ya kumpata hata yule ambaye alifikiria angemfaa katika maisha yake kimapenzi.

“Hiyo ilinigharimu sana maana mwisho wa siku walikuja kugundua na ilizua tafrani sana. Na hata kwa wakati mmoja waliungana dhidi yangu na unajua siku moja walikuja wote kwa pamoja.”

“Na katika mfarakano huo niliishia kumpoteza hata yule ambaye nilikuwa nafikiria alikuwa wangu wa kufaana naye. Na mwisho wa siku nilipoteza wote. Nilikuwa msichana mbaya. Na hicho ndicho kitu kimoja ambacho nisingependa wewe ufanye,” Diana alimaliza kwa ushauri.

Mama huyo wa watoto 3 alimshauri Morgan kujifunza kusema ‘hapana’ kwa vitu ambavyo havipendi ama vile ambavyo haviendani na falsafa yake ya maisha.