
MWANAHARAKATI wa haki za kibinadamu nchini Uganda, Winnie Byanyima amemsherehekea mumewe Kizza Besigye katika siku maalum ya kuzaliwa kwake.
Kupitia ukurasa wake wa X, Byanyima ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa shirika la UNAIDS Alifichua kwamba licha ya mumewe kuzuiliwa gerezani tangu Novemba mwaka jana na kunyimwa haki ya dhamana, hilo halizuii familia yake kusherehekea siku yake ya kuzaliwa.
Byanyima Alifichua kwamba Besigye ametimiza umri wa miaka 69 na kuweka wazi kwamba amekuwa mhibu wake kwa miaka 32 iliyopita.
“Heri ya kuzaliwa @kizzabesigye, rafiki yangu mpendwa na mshirika kwa miaka 32 iliyopita! Una miaka 69 leo. Umeishi maisha ya ujasiri, usadikisho, na kujidhabihu kama nini! Kupigania haki, uhuru, na utu kwa Waganda wote. Ninajivunia kutembea na wewe. Hapa ni kupenda, kusudi, na njia ngumu mbeleni. Tutashinda!” Byanyima alimsherehekea.
Besigye amesalia kizuizini tangu Novemba mwaka jana alipokamatwa kinyemela jijini Nairobi na kusafirishwa hadi Uganda alikozuiliwa katika gereza la kijeshi.
Hata hivyo baada ya pingamizi kadhaa, kesi yake ilihamishiwa katika mahakama ya kiraia mnamo Februari na kusomewa mashtaka ya uhaini ambayo adhabu yake ni kifo.
Hata hivyo, baada ya kukanusha, aliwekwa katika kizuizi cha gereza moja ambapo amekuwa akisota hadi sasa, baada ya wiki moja iliyopita kunyimwa dhamana tena.
Wafuasi wake ambao walisubiri kwa hamu uamuzi ambao ungemsaidia kiongozi huyo mkongwe kuachiliwa kwa dhamana waliachwa wakiwa wamekata tamaa baada ya Jaji anayesimamia kesi hiyo Rosette Comfort Kania kuamua vinginevyo.
Mara baada ya hakimu kumaliza kusoma uamuzi huo, wafuasi hao waliokuwa wamejaza chumba cha mahakama walianza kuimba kwa sauti kubwa, huku Besigye na washtakiwa wenzake wakijiunga kabla ya kusindikizwa kurudishwa gerezani.
"Tutashinda, tutashinda, naamini tutashinda siku moja," wafuasi hao waliimba kwa pamoja, huku wakiinua mikono juu kuungana na kiongozi wa upinzani.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!