
Mamlaka ya anga za mbali ya Kenya imetoa tahadhari kwamba huenda mabaki yatokayo anga za juu yakaanguka ardhini kati ya Jumamosi Aprili 19 na Jumapili Aprili 20.
Katika taarifa iliyotolewa jioni ya Ijumaa Aprili 18, KSA ilisema pia kwamba japo haijabainika wazi kwamba vitaanguka ndani ya ardhi ya Kenya, imewataka raia kuwa makini na kutoa ripoti ya tukio hilo mara moja kwa taasisi husika kama vile polisi.
Kifaa cha angani kinachotambuliwa kama Norad ID 61909/ 2024-205R ambacho ni kipande muhimu cha taka ama vifusi vya roketi iliyokuwa ikizunguka anga za mbali kinatarajiwa kupita katika anga ya eneo la Afrika Mashariki ikiwemo Kenya kati ya saa moja asubuhi za Jumamosi na saa tisa mchana ya Jumapili.
KSA imeongezea kwamba kifaa hicho kitapitia eneo la Kaskazini mwa jimbo la Kaskazini Mashariki mwa Kenya na kuelekea kusini mwa Kenya kuingia Tanzania.
Katika muda huu wa saa 24 kitazunguka anga ya juu ya eneo hili mara mbili ambapo inatarajiwa kwa kifaa hicho kuanguka ardhini.
KSA imeonya kwamba kitakuwa na madhara makubwa kwa maisha ya binadamu na wanyama na ni tishio kwa wanaoishi kwenye eneo ambapo msafara wa kifaa hicho utapitia.
Mwaka jana, kifaa kingine kilianguka katika kaunti ya Makueni nchini Kenya na japo hakikusababisha vifo vyovyote, kiliwatia wakaazi wa eneo hilo wasiwasi mkubwa kuhusu athari ya aina yoyote kutokana na wao kukigusa.
KSA ilikichukuwa kukifanyia uchunguzi wa kina katika maabara yao mjini Nairobi.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!