CRIME SCENE

Maafisa wa upelelezi wanachunguza mauaji ya kinyama ya watu watano wa familia moja waliouawa na wakazi wenye hasira katika wadi ya Masimba, Kaunti ya Kisii, kufuatia madai ya kuhusika kwao katika mauaji.

Kisa hicho kilitokea usiku wa Alhamisi katika kijiji cha Metembe, kulingana na ripoti ya polisi.

Katika shambulio hilo, kundi la wananchi pia liliwachomea nyumba sita zinazodaiwa kuwa za waathiriwa.

Polisi walisema kwamba watu wanne wa familia hiyo waliteketezwa hadi kufa, huku wa tano akikatwakatwa hadi kufa alipokuwa akijaribu kutoroka.

Ripoti za awali zinaonyesha kuwa wakazi walishuku familia hiyo kuhusika katika mauaji ya mwanamume wa makamo ambaye alipatikana ameaga mwezi mmoja uliopita.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Miongoni mwa waliouawa ni baba na mama wa familia hiyo. Hata hivyo, watu wengine wawili wa familia hiyo waliweza kutoroka wakiwa hai.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Kisii, Ronald Kirui, alithibitisha kuwa timu ya wachunguzi iko eneo hilo kuchunguza tukio hilo. Alilaani vikali kitendo hicho cha wananchi kujichukulia sheria mkononi, akikitaja kuwa ni uhalifu.

“Wanaoshukiwa wanapaswa kukabidhiwa kwa polisi ili wachunguzwe kisheria. Kikosi maalum kinaendelea kuchunguza mauaji haya,” alisema Kirui.

Polisi walifika kijijini humo siku ya Ijumaa asubuhi kama sehemu ya uchunguzi wa tukio hilo. Miili ya waathiriwa ilipelekwa katika mochari ya Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kisii kwa upasuaji na uchunguzi zaidi.

Kirui aliongeza kuwa maafisa wa DCI pia wanachunguza mauaji ya awali ambayo yanadaiwa kuchochea ghasia za Alhamisi.

Mashahidi walisema baadhi ya wakazi waliodaiwa kuhusika katika mauaji hayo walitoroka kijijini mara baada ya maafisa wa upelelezi kuwasili.

Polisi wameahidi kuhakikisha haki inatendeka kwa waathiriwa, na wakatoa onyo dhidi ya tabia ya watu kujichukulia sheria mkononi—tatizo sugu katika eneo hilo.

Viongozi wa usalama wanasema kuna uwezekano kuwa magenge ya wahalifu yaliyokuwa yakihangaisha eneo hilo yalihusishwa na mauaji hayo kabla ya juhudi za polisi kuimarishwa.

Aidha, uchunguzi umebaini kuwa baadhi ya waathiriwa walisingiziwa na kuuawa katikati ya mkanganyiko huo.