Jose Chameleone//INSTAGRAM

MSANII mkongwe wa tasnia ya kizazi kipya kutoka Uganda, Jose Chameleone amevunja kimya chake baada ya kurudi nyumbani akitokea hospitalini.

Msanii huyo amekuwa akipokea matibabu katika hospitali moja nchini Marekani kwa miezi kadhaa na wikendi iliyopita, alirejea nyumbani ambapo alilakiwa kwa shangwe na nderemo kutoka kwa familia na mashabiki wa muziki wake.

Chameleone kupitia Instagram yake, alianza kwak umshukuru Mungu huku akitangaza mabadiliko mapya ambayo ataanza kuyazingatia ili asije akarudi katika njia ya kulazwa hospitalini tena.

Kulingana naye, sasa na kwenda mbele atakuwa mwangalifu zaidi haswa katika suala la afya yake lakini pia atapunguza mafadhaiko na pia kuwaahidi mashabiki wake ujio wa miziki mingi mizuri kutoka kwake.

“Ahsante Mungu tumepita mabaya. Njia yangu mpya ni kuishi kwa afya. Bila mafadhaiko na kutengeneza muziki mwingi mzuri,” Chameleone aliandika.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Awali akizungumza na waandishi wa habari, Chameleone Alifichua kwamba licha ya kurejea nyumbani baada ya kulazwa kwa miezi 4, bado atakuwa anarejea Marekani kwa matibabu ya mara kwa mara.

Mwimbaji huyo alifichua hayo muda mfupi baada ya kurejea nchini Uganda, kufuatia kukaa kwa miezi minne nje ya nchi ambako alikuwa akipatiwa uangalizi maalumu.

Hata hivyo, alikiri kwamba bado hajapona kabisa.

"Bado sijapona… sijapona kabisa," aliwaambia wanahabari. "Nimerudi kwa sababu nilitamani nyumbani na nilihitaji kuwa hapa, lakini nitarejea Marekani karibu Mei 2 kwa ukaguzi."

Katika kikao hicho na wanahabari, Chameleone pia alikanusha uvumi kwamba afya yake ilikuwa na matatizo kutokana na unywaji wa pombe.

"Kuna idadi ya mambo, ikiwa ni pamoja na dhiki, DNA (genetics), na ukosefu wa usingizi," alifunguka.