
AFISA mmoja wa polisi ameripotiwa kuzirai na kufariki dunia baada ya kushuhudia timu ya Arsenal ikiicharaza Real Madrid 3-0 katika mkondo wa kwanza wa robo fainali ya kombe la klabu bingwa barani Ulaya, UCL.
Kwa mujibu wa jarida la PUNCH, Afisa wa Jeshi la Polisi nchini Nigeria kwa jina Inspekta Stephen Enang, alifariki dunia kwa msiba Jumanne usiku alipokuwa akitazama mechi ya UEFA Champions League kati ya Arsenal na Real Madrid kwenye kituo cha kutazama soka katika jimbo la Calabar.
Enang, mfuasi aliyejitolea wa Arsenal alifariki pindi tu baada ya kushuhudia timu yake ikiwaduwaza mabingwa mara 15 wa Champions League nyumbani.
Pia alisemekana kuwa hakuonyesha dalili zozote za ugonjwa kabla ya mchezo huo, na hata alijiunga na shangwe wakati bao la kwanza, la pili na la tatu la Arsenal lilipofungwa.
Kulingana na rafiki yake, ambaye hakutaka jina lake litajwe, inspekta marehemu aligunduliwa akiwa amepoteza fahamu baada ya filimbi ya mwisho.
"Kabla ya mechi, alikuwa mtu wa hali ya juu, hakukuwa na suala lolote tunalolijua, kwa sababu ni mtu mkimya na mpole, anapenda soka na ni shabiki wa Arsenal. Yeye ni Inspekta wa Polisi pia katika Kitengo cha Polisi Akim. Sote tulikuwa tunatazama mchezo, timu yake ilifunga bao la kwanza, na alifurahi sana na bao la pili na la 3.”
"Aliruka juu kwa shangwe kwa kila moja ya mabao haya; hatukujua kwamba alipokuwa ameketi nyuma kwenye kiti chake akisubiri filimbi ya mwisho, Stephen alikuwa hayupo. Tuligundua tu kwamba hakuwa akisogea baada ya mchezo, wakati kila mtu alikuwa akiondoka kwenye kituo cha kutazama, na hakusimama kama wengine.”
"Hapo ndipo tulipogundua kuwa hana fahamu tena, alikimbizwa katika hospitali ya Polisi ya Akim, ambapo wataalam wa afya walifanya kila wawezalo kumfufua, lakini juhudi zao zote ziliambulia patupu, kwani alithibitishwa kufariki."
Arsenal sasa wamo mguu mmoja ndani ya nusu fainali wakisubiria safari yao ya wiki ijayo nchini Uhispania kuchuana na Real Madrid katika mkondo wa pili.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!