Otile Brown

MSANII wa kizazi kipya, Otile Brown ameonyesha jinsi anavyomkosa mama katika maisha yake, akisema kwamba anachukia ukweli kwamba mamake hayupo hai leo hii kufurahia mafanikio yake.


Katika klipu fupi chenye hisia kali, msanii huyo alieleza kwamba mara kwa mara huwa anahisi pengo kubwa katika maisha yake ambalo liliachwa na mamake miaka kadhaa iliyopita.


Alieleza kwamba anatamani mamake angekuwa karibu naye leo hii kufurahia sehemu ya kile ambacho Mungu amembariki nacho.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans


“Nilirauka leo nikimpeza mamangu, nimekuwa nikilia siku nzima. Nachukia ukweli kwamba hayuko hapa leo hii kufurahia nasi hizi baraka kidogo ambazo Mungu ametubariki nazo,” Otile Brown alisema.


Alieleza kwamba angetamani sana mamake kuchuma matunda ya mafanikio ya wanawe, kwani walimshuhudia kabisa akiwahangaikia wakiwa Watoto.


“Nilimshuhudia mamangu akihangaika sana, alikuwa hustler wa kweli,” Otile Brown aliongeza kwa hisia.


Katika mahojiano na toleo la Pulse Magazine kwenye jarida la The Standard miaka 7 iliyopita, Otile Brown alifunguka kwamba alibaki yatima akiwa na umri wa miaka 14 wakati mamake alipoiaga dunia.


Msanii huyo anayetokea Pwani alifichua kwamba baada ya kufiwa, alilazimika kuuza chang’aa ili kujiendeleza kimaisha.


‘’Hata niliacha shule kwa sababu ya ukosefu wa karo. Mnamo 2013 niliamua kuhamia Nairobi kwa lengo la kujiimarisha katika tasnia ya burudani iliyokomaa,’’ Otile Brown alisema wakati wa mahojiano hayo.


“Nikiwa na imani na talanta, licha ya maisha magumu niliyokumbana nayo Nairobi ambayo yalinifanya nijitose katika kazi duni ikiwa ni pamoja na kuuza mitumba karibu na Chuo Kikuu cha Nairobi, sikukata tamaa katika ndoto yangu,’’ alisema.


Sasa msanii anayefanya vizuri, Otile anatamani mamake angekuwa hapa.


Mara kwa mara, Otile Brown amekuwa akionyesha mapenzi yake kwa marehemu mamake kwenye mitandao yake ya kijamii, akisimulia jinsi waliishi kwa furaha kabla ya umauti kumchukua.


‘’Nilipokuwa na umri wa miaka 14, siku moja kabla mama yangu hajafariki, Alinitazama machoni mwangu na kusema “Sina wasiwasi na wewe, utakuwa sawa.” Alikuwa na imani na mimi sana hivi kwamba ilibidi nijiamini hata zaidi. Tutakusherehekea daima mama .R.I.P,’ aliandika kwenye Instagram yake miaka 6 iliyopita.