Mbosso ashinda tuzo 3 katika hafla ya EAEA//INSTAGRAM

MBOSSO Khan, msanii wa Bongo Fleva amemaliza kile alichokitaja kama kasumba ya muda mrefu ya kutoshinda tuzo baada ya kujishindia tuzo 3 kwa mkupuo katika tafrija ya tuzo ya ukanda wa Afrika Mashariki iliyofanyika jijini Nairobi.

Katika hafla hiyo ya tuzo za EAEA ambayo ilifanyika usiku wa Jumatatu jijini Nairobi, Mbosso alikuwa akiwania tuzo katika vipengele vinne, na akaibuka mshindi katika vitatu kati yavyo.

Akizungumza baada ya ushindi huo, Mbosso alidai kwamba sasa anaweza furahi baada ya kasumba ya muda mrefu ya kutoshinda kura kumalizika rasmi.

Alisema kwamba kwa muda mrefu, amekuwa akitia fora katika utunzi wake wa muziki lakini hajakuwa na Bahati ya kushinda tuzo za maana, jambo ambalo alilitaja kama kasumba.

Alimalizia kwa kuwahongera mashabiki wake haswa kutoka Kenya na Tanzania kwa kuendelea kumpa sapoti ya kipekee hata baada ya kuwa msanii huru baada ya kuondoka WCB Wasafi yake Diamond Platnumz.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

“Nawashukuru sana na kwa wale mmenipigia kura Mungu awabariki sana. Nimekuwa na kasumba ya kukosa sana tuzo, kwa hiyo hii nafikiri mashabiki zangu watakuwa wamefurahi zaidi na zaidi.”

‘Tuendelee kusapotiana, Kenya, Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika yote kwa jumla, sisi wote ni wamoja ndio maana leo tuko hapa [Kenya] na tuna Imani siku nyingine pia mtakuja huko Tanzania,” Mbosso alisema.

Alisisitiza kwamba tuzo hizo 3 ni mahususi kwa minajili ya mashabiki wake ambao tangu kipindi anaitwa Marombosso walisimama naye na kipindi chote wametembea naye katika safari ya muziki hadi hapa anaposimama kama msanii huru.

“Hizi tuzo ni kwa ajili ya mashabiki wangu ambao siku zote wamekuwa wakitamani kuona nikipata tuzo. Kwa hiyo Mungu awabariki sana na ninashukuru zaidi,” alisema.

Mbosso amekuwa ni msanii wa 4 kuondoka katika lebo ya WCB Wasafi baada ya Harmonize, Rich Mavoko na Rayvanny kufanya hivyo miaka ya awali.

Kwa sasa, yeye ni msanii huru na wengi wana uchu kuona jinsi safari yake ya muziki itakavyoenda baada ya kung’atuka chini ya uongozi wa Diamond na timu yake.