
MSANII anayejitaja kama Tajiri zaidi katika sekta ya sanaa ya humu nchini, KRG the Don ametangaza kwamba huenda akajitosa katika sasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao 2027.
Katika mazungumzo na YouTuber Trudy Kitui, KRG alisema kwamba amechukua muda wake kuangalia jinsi siasa za taifa hili zinavyoendeshwa na ameridhika kwamba amekua kuingia katika dimbwi hilo.
Aliweka wazi kwamba wakati ataingia katika siasa, atawania ubunge japo hakusema ni eneo bunge lipi atalenga kuwakilisha bungeni baada ya Agosti 2027.
Mkwasi huyo alisema kwamba anajua fika siasa zinahitaji ukakamavu wa hali ya juu na kusema kwa jinsi amefuatilia siasa, anahisi kabisa mwili na akili zake ziko tayari kuwatumikia wananchi katika jumba la kutengeneza sheria.
“Nataka kugombea ubunge, lakini kwa sasa, sijaanza siasa tendaji. Siasa inachukua nguvu nyingi, na zaidi ya hayo, inadai kuwa wewe mwenyewe na kuelewa kile ambacho watu wanapitia. Nimechukua muda kujifunza mambo hayo, na niko tayari," KRG alijieleza.
Msanii huyo ambaye alipigwa vita vya mtandaoni na vijana wa Gen Z kutokana na misimamo yake mikali ya kusimama na rais Ruto wakati wengi walionekana kujitenga naye alitetea ukuruba huo akisema kwamba bado anaamini rais ndiye chaguo bora kwa taifa.
Kuhusu ni kwa nini hajateuliwa kwa wadhifa wowote serikalini licha ya kuitetea kwa udi na uvumba wakati asilimia kubwa ya vijana walionekana kuipinga kwenye maandamano, KRG alisema kwamba bado anasubiri na ana Imani siku yake inakuja.
Alieleza kwamba anajua uwezo wake katika kutekeleza majukumu mbalimbali na pengine jina lake litakapomfikia rais na amteua, atafanya kazi kwa ufasaha.
“Watu wengi walitarajia ningepewa wadhifa fulani, lakini unajua rais ndiye bosi na ndiye anayetathmini na kuona ni nani ana uwezo. Pengine jina langu bado halijafika kwenye orodha, lakini ikiwa atanipa nafasi ya kutumikia umma na nikapata nafasi hiyo, sijali. Najua ninaweza kufanya vizuri zaidi katika kazi kama hiyo,” alisema.
Mwaka jana baada ya kupapurana na watu mitandaoni, KRG alitangaza kuachana na kazi ya muziki kwa kile alichokitaja kuwa ni kupata muda zaidi wa kuzingatia biashara zake mbali na sanaa ya burudani.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!