
MWANAMUME mmoja kwenye mtandao wa TikTok amezua mjadala mkubwa baada ya kusimulia jinsi rafiki yake alijikuta kuwa mgeni wa mahabusu kisa mpenzi wake wa zamani.
Katika simulizi hiyo ambayo imegawanya watu kwa hisia na maoni tofauti, jamaa huyo alieleza kwamba rafiki yake amezuiliwa seli na anasubiri kufikishwa mahakamani baada ya kushtakiwa na mpenzi wake wa zamani.
Alieleza kwamba shtaka linalomkaili rafiki yake ni kujaribu kuchukua vitu vyote alivyomnunulia mwanamke huyo wakati wakiwa wapenzi kabla ya kuachana, ikiwemo simu.
Mwanamume huyo baada ya penzi kuisha, alitaka kurudishiwa kila kitu alichomfanyia mwanamke huyo, zikiwemo zawadi alizompa, lakini mrembo huyo hakuwa tayari kupoteza penzi na zawadi zilizotokana na mapenzi hayo, hivyo kumuitia polisi.
Msimuliaji alieleza: “Jamaa yangu alimnunulia mpenzi wake simu mwaka jana lakini wakati jamaa huyu alianza kuonyesha tabia za kumchosha mrembo wake, mrembo alienda akabadilisha ile simu na kununua nyingine tofauti kwa jina lake.”
“Wakati mwanamume huyo alirudi
kuchukua vitu vyake baada ya kuachana, akadai hiyo simu lakini mrembo akamuitia
polisi,” aliongeza.
Simulizi hii iliwachana mbavu baadhi ya watumizi wa mtandao wa TikTok, warembo wakionekana kumtetea mrembo huyo kwa kutorudisha simu na badala yake kumshtaki kwa polisi.
Kwa utetezi wao, walidai kwamba kitu chochote unachompa mtu wakati mkiwa katika uhusiano wa kimapenzi si deni wala kumuazima, bali ni cha kwake kihalali na endapo penzi litakwisha, huna haki yoyote ya kukirudia ama kukidai.
Kwa upande mwingine, wanaume walieleza kwamba jamaa huyo alikuwa na kila haki ya kutaka vitu vyake, kwani alikuwa amewekeza katika penzi hilo na kama limevunjika basi yuko huru kuondoka na hisa zake zote ili mwenye atakuja baadae aanze kutoka mwanzo kama alivyoanza yeye.
Je, ni sahihi kwa mtu kudai vitu alivyompa mpenzi wake penzi linapovunjika?
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!