
Afisa mmoja wa polisi aliwaua watoto wake watatu kabla ya kujitoa uhai ndani ya nyumba yake katika eneo la Rachuonyo, Kaunti ya Homa Bay.
Afisa huyo ambaye alikuwa ameajiriwa katika Kituo cha Polisi cha Marsabit, alikuwa amesafiri hadi nyumbani kwake siku ya Jumapili, Aprili 6, tukio hilo lilipotokea.
Marehemu ametambuliwa kama Konstebo David Okebe Goga wa kituo hicho cha polisi cha Marsabit.
Kwa mujibu wa polisi, walipata barua ya kujitoa uhai (suicide note) ndani ya nyumba hiyo, ambayo miongoni mwa maelezo yake, ilieleza namna yeye na watoto wake walipaswa kuzikwa.
Hata hivyo, maafisa hao walisema wanachunguza barua hiyo ili kubaini iwapo aliandika yeye binafsi.
Taarifa kutoka kwa polisi na majirani zinaeleza kuwa watoto waliouawa walikuwa ni wawili wa afisa huyo na mmoja aliyekuwa wa shemeji yake.
Watoto hao walikuwa ni mvulana wa miaka sita, msichana wa miaka mitano na mvulana mwingine wa miaka mitano wa shemeji yake.
Ripoti ya awali ya polisi inaonesha kuwa afisa huyo aliwalisha watoto hao sumu kabla ya yeye mwenyewe kujitia kitanzi ndani ya nyumba hiyo.
Tukio hilo lilitokea katika eneo la Kakdhimu Mashariki, eneo ndogo la Kawiti, kijiji cha Kawarwai, katika tarafa ya Rachuonyo Magharibi.
Sababu ya tukio hilo haijabainika mara moja, lakini polisi wamesema wameanzisha uchunguzi kamili kubaini kilichotokea.
Taarifa za tukio hilo zilisababisha mshtuko mkubwa na kutandaza huzuni miongoni mwa wakazi wa eneo hilo, huku umati mkubwa ukifurika nyumbani kwa marehemu.
Miili ya waathiriwa ilisafirishwa hadi mochari ambako inasubiri kufanyiwa upasuaji na taratibu nyingine za kitabibu.
Kisa hiki ni miongoni mwa matukio ya hivi karibuni yanayohusisha polisi kujitoa uhai.
Kwa mujibu wa maafisa wa usalama, visa vya polisi kujitia kitanzi vinaendelea kuongezeka licha ya juhudi mbalimbali za kukabiliana na hali hiyo, hali inayotajwa kuchangiwa na msongo wa mawazo.
Takwimu zinaonesha kuwa makumi ya polisi wamefariki dunia kwa kujitoa uhai au kuuawa, hali ambayo imehusishwa na mazingira magumu ya kazi.
Kama njia ya kukabili changamoto hiyo, mamlaka ya polisi imeanzisha huduma za ushauri nasaha huku Tume ya Huduma za Polisi ikianzisha kitengo maalum kilichopewa wahudumu wa kushughulikia afya ya akili miongoni mwa maafisa.
Kitengo hicho kinalenga kufanya tathmini, kuunda na kuendesha programu ya uhamasishaji inayolenga kuzuia matatizo ya afya ya akili na matumizi ya dawa za kulevya.
Kwa wastani, visa visivyopungua vitatu vya polisi kujitoa uhai huripotiwa kila mwezi. Maafisa wanasema kuwa polisi hupitia changamoto nyingi huku wakitarajiwa kudumisha sheria na utulivu hata katika mazingira magumu, sambamba na kuhatarisha maisha yao kazini.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!