
Mbunge wa Dagoretti North, Beatrice Elachi, amethibitisha kuwa mwanaye, Elvis Murakana Namenya, alifariki kutokana na majeraha mabaya ya kichwa baada ya kuhusika katika ajali mbaya ya barabarani.
Akizungumza katika ibada ya kumbukumbu iliyofanyika katika Kanisa la Holy Trinity, Kileleshwa, Ijumaa, Machi 27, mwanasiasa huyo wa ODM alieleza kwa kina namna ajali hiyo ilivyotokea, akifichua kuwa Elvis alipata jeraha kubwa kichwani lililosababisha ubongo wake kuathirika vibaya.
Kwa mujibu wa Elachi, Elvis alikuwa akirejea nyumbani baada ya kukutana na rafiki yake alipokumbwa na tatizo la gurudumu kutoboka ghafla. Kwa kushindwa kuidhibiti hali hiyo, gari lake liligonga vibaya, na majeraha aliyoyapata yakapelekea kifo chake.
“Nataka kuzungumza na wazazi kuhusu watoto wetu leo. Tuna kizazi kinachoamini kuwa kinaweza kushughulikia changamoto zao peke yao. Wanaweza kuamka muda wowote kusaidiana bila hata kutufahamisha. Watatuambia tu ikiwa hawawezi tena kusuluhisha hali hiyo. Lakini wanasaidiana sana, na mara nyingine hata hatujui kinachoendelea,” alisema.
Mbunge huyo alitumia fursa hiyo kuzungumzia usalama barabarani, hasa jinsi ya kushughulikia pancha wakati wa kuendesha gari.
“Elvis alikuwa tayari amelala saa nne na nusu usiku alipigiwa simu kuhusu kazi fulani. Alienda haraka na kuimaliza. Lakini alipokuwa akirejea, gari lake likapata pancha. Vijana wengi hawajui kuwa gari likipata pancha, hupaswi kabisa kubana breki za dharura. Gari litatereza, na hapo ndipo unaweza kupoteza mwelekeo kabisa. Unachopaswa kufanya ni kushikilia usukani kwa nguvu, kuhakikisha gari linapunguza mwendo polepole, na kumwomba Mungu lisimame salama. Kwa bahati mbaya, Elvis alipata jeraha baya sana—ubongo wake ulitoka mahali pake, na hilo ndilo lililosababisha kifo chake,” alieleza.
Elachi alisimulia pia jinsi alivyomtazama mwanaye akiwa ICU siku ya Jumamosi na kufahamu kuwa hangeweza kupona.
"Sikuambia hata madaktari, lakini nilipomtazama, nilijua tu—anaenda zake," alisema kwa huzuni.
Akimzungumzia marehemu mwanaye, mbunge huyo alisema Elvis alikuwa kijana aliyependa sana kanisa, muziki, na soka. Ingawa alikuwa mtu wa kujitenga, alipenda sana mpira wa miguu, na kadri alivyokua, alipata mapenzi makubwa kwa muziki
"Lakini jambo moja nitawaambia, alipenda sana kanisa hili. Na hata ninapokuja hapa, ukiwauliza watu wa Holy Trinity, sijawahi kuja kama 'Mheshimiwa'," aliongeza.
Elachi alihitimisha kwa kumwomba Mungu amrehemu na kumfungulia Elvis mlango wa mbinguni, ili apate pumziko la milele.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!