
Serbia imekashifu vikali hatua ya Kenya kutambua rasmi uhuru wa Kosovo, ikisema uamuzi huo unakiuka sheria za kimataifa na unahujumu moja kwa moja Azimio Namba 1244 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Kupitia Wizara yake ya Mambo ya Nje, Serbia ilisema kwa kutambua uhuru wa Kosovo, Kenya imeenda kinyume na makubaliano ya kimataifa yanayohakikisha kuwa eneo hilo bado ni mali ya Serbia
"Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Serbia inalaani vikali uamuzi wa Jamhuri ya Kenya wa kutambua uhuru wa upande mmoja wa kile kinachoitwa 'Kosovo'," ilisema taarifa hiyo.
Serbia ilisisitiza kuwa hatua hiyo imechukuliwa mwaka huu ambapo dunia inaadhimisha miaka 80 tangu kupitishwa kwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa, mkataba ambao Kenya "imepuuza" kwa kufanya uamuzi huo.
Aidha, serikali ya Serbia ilisema hatua hiyo inadhoofisha juhudi za kukuza mazungumzo yenye tija, kuimarisha uthabiti wa kanda, na kuheshimu utaratibu wa kimataifa wa kisheria.
Serbia pia ilikosoa rejeleo lolote kwa uamuzi wa 2010 wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kama msingi wa kuhalalisha hatua ya Kenya, ikisema hoja hiyo haina msingi wowote wa kisheria.
Nchi hiyo ilieleza masikitiko yake kwamba uamuzi wa Kenya unaathiri uhusiano wa muda mrefu kati ya mataifa haya mawili, uhusiano ambao umejengwa kwa heshima na ushirikiano wa miaka mingi, hasa kupitia Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (Non-Aligned Movement).
Serbia ilionya kuwa itachukua hatua zote za kidiplomasia na kisiasa kujibu "kitendo hiki kisichokubalika na kisichokuwa cha kirafiki."
Serikali ya Serbia pia ilibainisha kuwa katika miaka minane iliyopita, mataifa 28 yamefuta au kusimamisha utambuzi wao kwa uhuru wa Kosovo, huku ni nchi mbili pekee zikiutambua.
Serbia ilisisitiza kuwa jumuiya kubwa ya kimataifa inaendelea kuunga mkono msimamo wake, ikidai kuwa sheria na haki vinaegemea upande wake.
"Jamhuri ya Serbia itaendelea kulinda mamlaka na uadilifu wake wa ardhi kwa kutumia njia zote za kidiplomasia na kisheria," ilisema taarifa hiyo.
Kenya ilitangaza kutambua rasmi uhuru wa Kosovo siku ya Jumatano, na kuwa nchi ya kwanza kufanya hivyo baada ya takriban miaka mitano ya mkwamo katika juhudi za Kosovo kupata utambuzi zaidi kimataifa.
Hatua hiyo ilithibitishwa na Rais wa Albania, Bajram Begaj, baada ya mkutano kati ya Mjumbe Maalum wa Kosovo, Behgjet Pacolli, na Rais wa Kenya, William Ruto, jijini Nairobi.
"Furaha yangu kubwa kuona Kenya imetambua taifa la Kosovo leo. Namshukuru rafiki yangu Rais William Ruto kwa uamuzi huu, ambao umeungwa mkono kwa moyo mkunjufu na Waalbania wote," Begaj aliandika kwenye X.
Kosovo ilijitangazia uhuru wake kutoka Serbia mwaka 2008, lakini haijawa mwanachama wa Umoja wa Mataifa kutokana na upinzani kutoka Serbia na washirika wake, ikiwemo Urusi na China ambazo zina kura ya turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Hadi sasa, zaidi ya mataifa 110, yakiwemo Marekani na nchi nyingi za Ulaya, yametambua uhuru wa Kosovo.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!