
SHIRIKISHO la soka humu nchini, FKF limetoa taarifa muda mfupi baada ya kusambaa kwa video zikimuonyesha aliyekuwa mlinda lango wa timu ya taifa Patrick Matasi kudaiwa kuhusika katika upangaji wa matokeo.
Katika video hizo, Matasi ambaye wiki chache zilizopita alihamia klabu ya Kakamega Homeboyz akitokea Police FC alionekana akifanya mazungumzo na mtu asiyeonekana.
FKF katika taarifa yao wametaja kwamba wameiona video hiyo inayobeba madai mazito kumhusisha Matasi na kula njama ya kupanga matokeo na kuthibitisha kuwa uchunguzi umeanzishwa.
“FKF imefahamishwa kuhusu video zinazosambwa mitandaoni zikimhusisha mlinda lango Patrick Matasi, na kuibua madai kuhusu uwezekano wa kuhusika katika upangaji matokeo.”
“FKF inashikilia uadilifu wa soka na imeanzisha uchunguzi kwa kushirikiana na FIFA, CAF na Idara nyingine husika. Tunasisitiza sera yetu ya kutovumilia upangaji wa matokeo na tunajitolea kulinda uhalali wa mashindano.”
Aidha, shirikisho hilo liliahidi uchunguzi wa haki na uwazi na kusisitiza kwamba haki za Matasi na klabu anayoitumikia kwa sasa ya Kakamega Homeboyz zinalindwa na kuheshimiwa wakati wote wa uchunguzi.
“Uchunguzi huu utaendana na kanuni ya kupinga upangaji wa matokeo na mwongozo wa FIFA ili kuhakikisha mchakato wa haki, uwazi na wa kina. Haki za mchezaji na klabu yake zitaheshimiwa na hatua madhubuti zitachukuliwa kulingana na matokeo ya uchunguzi,” FKF iliongeza.
Shirikisho pia lilitoa wito kwa mtu yeyote mwenye ana ushahidi zaidi ya kufanikisha uchunguzi huo kujitokeza na kutoa taarifa kwao.
“Tunatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa za kuaminika kusaidia katika uchunguzi huu. Taarifa zote zitashughulikiwa kwa usiri wa kipekee,” FKF ilisema huku ikitoa barua pepe ya kutumwa kwa taarifa hizo.
Mlinda lango huyo aliyechujwa kutoka kwa kikosi cha timu ya taifa na kocha mpya Benni McCarthy alihamia klabu ya Homeboyz mwezi Februari akitokea klabu ya Police FC.
Awali, Matasi aliwajibika katika klabu ya Tusker baada ya kurudi nyumbani kutoka St George ya Ethiopia.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!