
Bi Mellen Mogoka, mwanamke anayedaiwa kushambuliwa kwa kukataa kutupa mchanga kwenye kaburi la mume wake wa zamani katika eneo la Nyabisimba, Kaunti ya Nyamira, ameibuka na kusimulia kuhusu tukio hilo la kutisha.
Akizungumza na mwanahabari akiwa nyumbani kwao Narok, Mellen alifichua kuwa alikataa kushiriki katika mila hiyo kutokana na uhusiano mgumu aliokuwa nao na baba wa watoto wake, hali iliyosababisha ndoa yao kuvunjika.
Alisisitiza kuwa licha ya kumheshimu mumewe huyo wa zamani, alimtesa sana wakati wa ndoa yao, jambo lililomfanya kuchukua uamuzi wa kutotupa mchanga kaburini mwake.
"Kulingana na jinsi tulikuwa tumesumbuana na huyu baba watoto wangu, heshima nilikuwa nimempa, lakini maneno yote alikuwa akinifanyia, nilikuwa nimevumilia mpaka nikasema hakuna vile nitamrushia mchanga," alisema Mellen.
Mwanamke huyo alieleza kuwa alikuwa ameonywa kuwa kutupa udongo kaburini kwa mume wake wa zamani kungezuia kusonga mbele na maisha yake.
Alisema kuwa alipoamua kutoshiriki katika mila hiyo, wakwe zake walianza kumshutumu kwa kudai kuwa alihusika na kifo cha mume wake wa zamani, madai anayoyakana vikali.
"Vile waliniambia kurusha mchanga utakuwa umejifunga, hakuna mahali nitawahi kuenda maishani. Watoto wangu ni wadogo, mimi bado ni mdogo. Walianza kuniambia ‘ni wewe umemuua,’ nikawaambia mhubiri ako hapa, naweza chukua Biblia na nisimame mbele ya kaburi yake na waniombee. Kama nimefanya kitu kama hiyo, hata na mimi nimfuate," alisimulia.
Mellen aliendelea kusisitiza kuwa hana uhusika wowote katika kifo cha mume wake wa zamani.
"Sijamuua. Mahali alipata ajali sio huku Narok. Alipata ajali akiwa kwao, sio mimi. Wakauliza kwa nini sitaki kurusha mchanga kama sio mimi nimemuua? Wakasema na juu tulikuwa tunasumbuana, hakuna mahali nitawahi kuoleka," aliongeza.
Siku ya Jumanne, polisi waliwakamata washukiwa watatu kuhusiana na tukio hilo.
Washukiwa hao walidaiwa kumlazimisha Mellen kushiriki katika mila za kitamaduni, kinyume na matakwa yake, kabla ya kumvamia na kumsababishia majeraha mwilini.
Tukio hilo linaripotiwa kutokea mnamo Machi 21, 2025, wakati mwanamke huyo aliyekuwa ameolewa na marehemu kwa zaidi ya miaka tisa, aliwasili kwenye mazishi yake kufuatia mwaliko wa mama mkwe wake.
Mwanamke huyo alikuwa ametengana na marehemu kwa muda mrefu na hakuwa na mawasiliano naye hadi alipofariki dunia katika ajali ya barabarani.
Kwa mujibu wa taarifa za polisi, hali ilibadilika ghafla wakati wa mazishi, baada ya baadhi ya jamaa wa marehemu kumtaka atimize desturi ya kutupa mchanga kaburini.
Mwathiriwa alipokataa, inadaiwa kuwa walimshutumu kwa kusababisha kifo cha mumewe wa zamani na kisha wakamshambulia vikali mbele ya waombolezaji.
Maafisa wa polisi walifahamishwa kuhusu tukio hilo na kuanzisha msako mara moja.
Hatimaye, washukiwa hao walikamatwa katika eneo la Mwongorisi na kupelekwa katika Kituo cha Polisi cha Kiambere kwa uchunguzi zaidi kabla ya kufikishwa mahakamani.
Wakati huo huo, juhudi za kuwatambua na kuwakamata washukiwa wengine wanaohusishwa na shambulio hilo zinaendelea.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!