
Programu hiyo, inayojulikana kama CBP Home, inawaruhusu wahamiaji kusajili "dhamira yao ya kuondoka," ambapo Idara ya Forodha na Doria ya Mipaka ya Marekani, inasema inawapa nafasi ya kuondoka bila ya kuondoshwa kwa nguvu.
Maafisa wa Marekani wameendelea kusema mara kwa mara kwamba wahamiaji wasio na vibali nchini humo wanapaswa kuondoka kwa hiari, badala ya kukamatwa na kufukuzwa.
Hii ni hatua ya hivi punde zaidi katika juhudi za Ikulu ya White House ya kurekebisha mfumo wa uhamiaji wa Marekani, ili kuendana na ahadi za Trump, ikiwemo kuwahamisha watu wengi kwa nguvu.
Katika taarifa yake, Katibu wa Usalama wa Ndani, Kristi Noem amesema kwa kuondoka wenyewe nchini kupitia programu hiyo, wahamiaji "watakuwa na fursa ya kurejea kisheria katika siku zijazo na kuishi Marekani."
"Ikiwa hawatafanya hivyo, tutawatafuta, tutawafukuza na hawatarejea tena," aliongeza.
Programu pia inawauliza wahamiaji kama wana "fedha za kutosha kuondoka Marekani" na ikiwa wana "pasipoti halali, ambayo muda wake haujaisha kutoka nchi yao ya asili."
Utawala wa Trump ulifanya haraka kufuta programu ya CBP One kama sehemu ya mabadiliko katika sera zake za uhamiaji. Pia ilisitisha ruhusa kwa wahamiaji wasio na vibali kuingia Marekani, na kuongeza kamatakamata ya wahamiaji kupitia Idara ya Uhamiaji na Forodha (ICE).
Takriban watu 30,000 walisemekana kukwama ndani ya Mexico tangu programu hiyo ilipoondolewa - wote wakiwa na miadi ambayo sasa imeghairishwa.
Kabla ya agizo hilo, wahamiaji waliweza kufika kwenye mpaka wa Marekani na walikuwa na haki ya kisheria ya kuomba hifadhi.
Trump pia amesitisha mpango wa kuwapatia wakimbizi makazi mapya Marekani. Chini ya utawala wa Joe Biden mwaka 2024, Marekani ilikubali zaidi ya wakimbizi 100,000 - idadi kubwa zaidi tangu 1995.
Mwishoni mwa Februari, utawala wa Trump ulisema utaunda daftari la kitaifa kwa wahamiaji wasio na hati na ambao watashindwa kujiandikisha wanaweza kukabiliwa na mashtaka ya jinai.
Kuna takriban wahamiaji milioni 13 wasio na vibali nchini Marekani. Haijulikani ni wangapi watasajili au wataathiriwa na agizo la usajili.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!