Wema Sepetu

MUIGIZAJI wa muda mrefu wa filamu za Bongo, Wema Sepetu amefichua kwamba yeye anamzidi mpenzi wake, mwanamuziki Whozu kwa miaka 6.

Akizungumza na waandishi wa habari za burudani wakati wa kusherehekea siku ya kuzaliwa ya Whozu, Wema alikanusha tetesi kwamba anamzidi Whozu jumla ya miaka 15.

Hata hivyo, alisema kwamba haoni tatizo kuwa katika uhusiano wa mapenzi na mwanamume ambaye ni mdogo kiumri, akitetea pengo la miaka 6 baina yao.

Kwa mujiu wa Sepetu, pengo la miaka 6 baina yake na Whozu si vibaya sana kwani kuna baadhi ya wapenzi ambao wana pengo la hadi miaka 20 kati yao na mapenzi yanataradadi vyema tu.

Muigizaji huyo alifichua kwamba wamekaa katika uhusiano wa kimapenzi na Whozu kwa miaka 4 sasa ila akawarai mashabiki wao wanaotamani kushuhudia harusi yao kusubiri kwa kitambo kidogo.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

“Mimi Whozu namzidi kwa miaka 6 na wala si 15. Nimemzidi miaka 6 ambayo kwangu mimi naona sio mibaya sana hata kama ingekuwa 10 kwani shida iko wapi? Kuna watu wengine huko wamezidiana kwa miaka 20-25, sembuse mimi miaka 6 tu!” Sepetu alisema kwa kujishaua.

“Tuna miaka 4 sasa ya hivi katika uhusiano, labda niseme hivi kwamba mimi ndoa sio kitu ambacho nakiota wala kukitamani sana, kwa sababu pia nimeona imeniharibu kisaikolojia watu wangu wa karibu, ndugu zangu, rafiki zangu nimewaona ndoa zikiwaharibikia.”

“Kwa hiyo sijui nimekuwa ni muoga lakini mimi nahisi ndoa ni mipango ya Mungu, kama Mungu kawaandikieni ndoa itakuwa tu, si kitu cha kulazimisha. Cha kushukuru Mungu ni kwamba kuna upendo ndani mwetu na siku hizi wanasema kwamba mkishaishi pamoja miezi 3 tayari ni kama mmeoana,” Wema Sepetu alisisitiza.

Wema alitetea uhusiano wake na Whozu akisema kuwa mtu yeyote hata kutoka kwa familia yake ambaye ana shida na uhusiano wake na Whozu basi nilo ni kwao wala si kwake.

Alirejelea tukio la miaka miwili iliyopita ambapo mamake alifoka vikali kukata uhusiano wa bintiye na Whozu ambaye alimuona kama kijana ambaye hajakomaa kuwa katika penzi na mwanawe.