
Naibu Rais Kithure Kindiki, ameonya kuwa taifa haliwezi kusonga mbele iwapo wananchi wataendelea kudharau au kutochukulia kwa uzito juhudi zinazofanywa na serikali katika kukuza uchumi na maendeleo.
Akizungumza katika mji mkuu wa Namibia, Windhoek, wakati wa mkutano na wataalamu wa jamii ya Wakenya wanaoishi nchini humo, Kindiki alisisitiza kuwa mafanikio makubwa yanaweza kupatikana iwapo wananchi watajitolea na kushirikiana katika miradi inayolenga kuleta maendeleo.
Huku akitoa mfano, alisema kuwa kuna kampuni kadhaa ambazo zimeonyesha nia ya kuwekeza katika Eneo la Viwanda vya Ngozi la Kenya (KLIP) lililoko Kenanie, Athi River, lakini baadhi ya Wakenya bado hawaamini kuwa mradi huo ni halisi.
Alihusisha hali hiyo na mtazamo wa baadhi ya wananchi wa kutokuwa na imani na miradi mikubwa, hali ya kutoridhika na kutofikiria mbali.
"Tuna wawekezaji 32 walioonyesha nia ya kushiriki katika mradi huu, lakini kwa bahati mbaya, kuna Wakenya wanaodhani haya ni maneno matupu. Hii ni kwa sababu wengi wamezoea hali ya kutoamini mambo makubwa yanawezekana nchini," alisema Kindiki.
Hata hivyo, Kindiki alisisitiza kuwa hata kama si kila mwekezaji ataingia sokoni, hata wachache wakianza kazi, manufaa makubwa yataonekana. Aliweka wazi kuwa uwekezaji huu utaongeza thamani ya bidhaa za ngozi, kuongeza ajira, na kuimarisha uchumi wa taifa.
"Tusipojipanga vizuri, tunaweza kupoteza fursa hii kubwa. Lakini tukiamka, tutaona viwanda vinavyochakata ngozi, ajira zikiongezeka, na bidhaa zetu zikishindana katika soko la kimataifa. Lazima tubadili mtazamo wetu na tuache kufikiria kwa kiwango kidogo."
Kindiki aliongeza kuwa serikali inatarajia KLIP kuzinduliwa ifikapo Juni 2025.
Kwa mujibu wake, mradi huo unalenga kuongeza idadi ya ajira katika sekta ya ngozi kutoka nafasi 17,000 za sasa hadi takriban 150,000.
Alibainisha kuwa wawekezaji hao wanakuja kuleta mfumo wa kisasa wa usindikaji wa ngozi ili kuzuia upotevu wa malighafi muhimu.
"Kwa sasa, ngozi nyingi za mifugo zinatupwa ovyo au kuachwa kuliwa na wanyama pori, lakini ukweli ni kwamba ngozi ina thamani kubwa kuliko hata nyama. Tunapaswa kuelewa kuwa bidhaa za ngozi, kama viatu tunavyovaa, vina thamani kubwa katika soko la kimataifa, na tunaweza kunufaika zaidi tukitumia rasilimali hii ipasavyo," alisema.
Naibu Rais amekuwa nchini Namibia kwa ziara rasmi ya siku tatu.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!