
Kiongozi wa Kanisa Katoliki, Papa Francis, anaendelea kupata nafuu baada ya kulazwa kwa wiki mbili katika Hospitali ya Gemelli mjini Roma kwa ajili ya matibabu ya nimonia ya mapafu yote mawili.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Habari ya Vatican Ijumaa asubuhi, Februari 28, ilieleza kuwa Papa alipata usingizi mzuri usiku wa 15 hospitalini
“Kama ilivyokuwa katika siku za hivi karibuni, usiku umepita kwa utulivu, na Papa kwa sasa anapumzika,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Papa Francis alilazwa Februari 14 baada ya kugunduliwa na maambukizi ya njia ya upumuaji, ambayo baadaye yaligeuka kuwa nimonia sugu inayojulikana kama bilateral pneumonia.
Tangu wakati huo, amekuwa akipokea matibabu maalum, yakiwemo matumizi ya oksijeni ya mtiririko wa juu na tiba ya kupumua.
Taarifa ya Alhamisi jioni ilieleza kuwa hali yake inaendelea kuimarika, ingawa madaktari bado wanachukua tahadhari.
“Hali yake ya kiafya inaendelea kuboreka, ingawa bado ni tete. Matibabu yanaendelea,” ilisema Vatican.
Licha ya changamoto za kiafya, Papa Francis ameweza kushiriki katika shughuli mbalimbali kutoka hospitalini, ikiwa ni pamoja na kuteua maaskofu wapya.
Hata hivyo, Vatican imefuta matukio kadhaa aliyokuwa amepanga kufanya, kama sala ya Malaika wa Bwana Jumapili, ili kumpa muda wa kupona.
Papa Francis, mwenye umri wa miaka 88, ana historia ya matatizo ya mapafu, kwani sehemu ya pafu lake iliondolewa alipokuwa kijana. Licha ya hali hiyo, amekuwa akiendelea na majukumu yake kwa ari na ujasiri.
Waumini wa Katoliki kote duniani wanaendelea kumuombea kiongozi wao apone haraka, huku Vatican ikiendelea kutoa taarifa za maendeleo yake.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!