
Mamlaka ya Barabara Kuu Nchini Kenya (Kenha) imewatangazia watumiaji wa barabara kuhusu usumbufu wa trafiki unaotarajiwa kwenye mzunguko wa Haile Selassie jijini Nairobi.
Hali hii itaathiri eneo hilo kuanzia Machi 3 hadi Aprili 7, 2025, ili kutoa nafasi kwa ujenzi wa njia maalum ya waenda kwa miguu chini ya barabara (underpass).
Kwa mujibu wa Kenha, hatua hii ni sehemu ya juhudi za kuboresha miundombinu ya mijini na kuhakikisha usalama wa waenda kwa miguu kwa kuwaondoa kutoka barabarani.
"Tunafahamu kuwa mabadiliko haya yatasababisha usumbufu kwa muda, lakini tunawaomba madereva na waenda kwa miguu kushirikiana nasi kwa kufuata mpangilio wa trafiki uliopangwa na maafisa husika," alisema Mkurugenzi Mkuu wa Kenha, Eng. Kung’u Ndung’u.
Mradi huu ni sehemu ya ujenzi wa mtandao wa Njia ya watembea miguu kupitia chini ya Greenpark, unaosimamiwa na Mamlaka ya Barabara za Mijini (KURA) kwa gharama ya Sh2 bilioni.
Ujenzi huu unalenga kurahisisha usafiri wa waenda kwa miguu wanaovuka Barabara kuu ya Uhuru kuelekea Upper Hill na maeneo ya karibu bila kuathiri mtiririko wa magari.
Katibu wa Wizara ya Barabara, Joseph Mbugua, amefichua kuwa underpass hii itakuwa na maduka yatakayofanya kazi muda wote wa saa 24, hatua inayolenga kuongeza shughuli za kiuchumi na kuimarisha usalama katika eneo hilo.
"Tumehakikisha kuwa sehemu ya mradi huu inajumuisha biashara ndogo ambazo zitakuwa wazi hadi usiku. Hii itasaidia kuvutia uwepo wa polisi na hivyo kuimarisha usalama wa waenda kwa miguu," alisema Mbugua.
Madereva na watembea kwa miguu wanashauriwa kufuata maelekezo ya trafiki yaliyowekwa na kushirikiana na maafisa wa usimamizi wa barabara ili kupunguza msongamano wa magari na hatari za usalama.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!