
Mchezaji wa zamani wa Barcelona, Gerard Piqué, ametoa pendekezo la mageuzi makubwa katika soka
Gwiji huyo wa soka mwenye umri wa miaka 38 amependekeza kwamba iwapo mechi itamalizika kwa sare ya 0-0, basi hakuna timu inayopaswa kupewa pointi yoyote.
Piqué alitoa wazo hili wakati wa mazungumzo na mlinda mlango wa zamani wa Real Madrid, Iker Casillas, kwenye podikasti ya Casillas.
Kwa mujibu wa Piqué, lengo ni kuongeza ushindani na burudani katika soka, kwani mashabiki hulipa pesa nyingi kuhudhuria mechi na wanapaswa kufurahia mpira wa kuvutia wenye mabao.
“Mashabiki wanapokuja uwanjani au kutazama mechi kwenye televisheni, wanataka kuona burudani. Kama timu hazifungi mabao, basi hakuna sababu ya kuwapa pointi,” alisema Piqué.
Mbali na kuondoa pointi kwa sare ya 0-0, Piqué pia amependekeza soka liondoe sare kabisa.
Anahoji kuwa michezo kama mpira wa vikapu (basketball) na baseball hazina sare, hivyo hata soka linapaswa kufuata mkondo huo.
Katika jitihada zake za kuboresha burudani katika soka, Piqué ameanzisha Kings League, mashindano ya soka la wachezaji saba kwa kila upande. Mechi za ligi hiyo huchukua dakika 40 pekee na zikimalizika kwa sare, mshindi huamuliwa kupitia mikwaju ya penalti.
Ligi hiyo pia inatumia kanuni za kipekee, kama vile kutumia kadi maalum zinazotoa faida au adhabu kwa timu fulani ndani ya mchezo.
Mfano, kadi moja inaweza kuruhusu timu kuondoa mchezaji wa mpinzani kwa muda fulani, au kupewa penalti ya moja kwa moja.
Pendekezo la kuondoa sare za 0-0 kwa kutotoa pointi kwa timu zote mbili linaweza kuwa na athari kubwa kwa soka. Ingawa baadhi ya mashabiki wanaweza kulikubali kwa sababu litahamasisha mashambulizi zaidi na soka la kusisimua, wengine wanaweza kuliona kuwa hatari kwa mbinu za uchezaji, hasa kwa timu zinazotegemea ulinzi thabiti.
Katika historia ya soka, sare za 0-0 zimekuwa sehemu ya mbinu, hasa katika mashindano makubwa kama Kombe la Dunia na Ligi ya Mabingwa. Timu nyingi hutumia sare kupata pointi muhimu, hasa zinapokutana na wapinzani wenye nguvu.
Hata hivyo, Piqué anaamini kuwa soka lazima libadilike ili kuwavutia mashabiki wapya, hasa kizazi cha vijana ambacho kina mwelekeo wa kuvutiwa na burudani za kasi na msisimko.
Bado haijulikani iwapo FIFA au mashirikisho ya soka kama UEFA yatazingatia pendekezo lake, lakini mjadala kuhusu mustakabali wa sare za 0-0 umeanza kushika kasi miongoni mwa wadau wa soka duniani.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!