Lionel Messi na Luis Suarez

Mshindi wa Kombe la Dunia mwaka wa 2022, Lionel Messi, pamoja na mshambuliaji mwenzake wa Inter Miami, Luis Suárez, wamepigwa faini na Major League Soccer (MLS) kwa kukiuka sheria za ligi hiyo zinazokataza kushika uso, kichwa au shingo ya mpinzani.

Tukio linalomhusisha Messi lilitokea mwishoni mwa mechi ya Inter Miami dhidi ya New York City FC iliyomalizika kwa sare ya 2-2 mnamo Februari 22.

Messi alionekana akimkabili kocha msaidizi wa New York City, Mehdi Ballouchy, mara baada ya filimbi ya mwisho. Katika tukio hilo, Messi alishikwa na hasira na kumwekea mkono Ballouchy shingoni mara mbili, hali iliyosababisha mzozo mkali kati yao.

Kabla ya kisa hicho, Messi alikuwa tayari ameonyesha kutoridhishwa na maamuzi ya mwamuzi Rosendo Mendoza na hata akapewa kadi ya njano kwa malalamiko yake alipokuwa akielekea kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.

Mbali na Messi, Suárez naye alipigwa faini kwa kosa sawa na hilo, baada ya kumbana shingoni beki wa NYC FC, Birk Risa, wakati wa mapumziko ya kipindi cha kwanza.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Hata hivyo, MLS haijafichua kiasi halisi cha faini walizotozwa wawili hao.

Katika taarifa yao, MLS ilisema kuwa kamati yao ya nidhamu ilibaini kuwa nyota hao wawili wa zamani wa Barcelona walivunja sheria ya ligi inayopinga kushika uso, kichwa au shingo ya mpinzani.

Messi alikuwa na mchango mkubwa katika mchezo huo kwa kutoa pasi ya bao lililofungwa na Telasco Segovia katika muda wa nyongeza, likisaidia Inter Miami kupata sare. Pia, alitoa pasi nyingine ya bao kwa mchezaji Tomas Avilés, ambaye baadaye alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumuangusha mshambuliaji wa NYC FC, Alonso Martínez, aliyekuwa anaelekea kufunga.

Adhabu hii inakuja siku chache baada ya tukio jingine lililomhusisha Messi na waamuzi. Mwamuzi wa mchezo wa Inter Miami dhidi ya Sporting Kansas City katika michuano ya Concacaf Champions League alisimamishwa kwa miezi sita baada ya kuomba jezi ya Messi baada ya mechi. Katika mchezo huo, Messi alifunga bao pekee lililoipa Miami ushindi wa 1-0 katika mazingira ya baridi kali huko Kansas City.

Adhabu dhidi ya Messi na Suárez zinaashiria msimamo mkali wa MLS kuhusu nidhamu ya wachezaji, huku ligi hiyo ikionyesha kuwa haitavumilia vitendo vinavyokiuka kanuni zake.