Crime scene

Polisi wa kupambana na ugaidi mnamo Jumanne asubuhi waliwakamata washukiwa wawili wa kundi la Al Shabaab katika kaunti ya Mandera.

Wawili hao wanaripotiwa kuwa walikuwa wakipanga utekaji nyara wa raia wa kigeni waliokuwa wakifanya kazi kwenye mradi wa ujenzi wa mtaro wa maji taka katika mji wa Mandera.

 

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), msako wa kiintelijensia uliongoza maafisa wa usalama kumkamata mshukiwa mkuu, Isaac Abdi Mohamed, anayejulikana pia kama Kharan Abdi Hassan, mwenye umri wa miaka 29.

 

Inadaiwa kuwa alijipenyeza nchini hivi majuzi kutoka El-Ade, Somalia, na kutengeneza stakabadhi ghushi ili ajitambulishe kama Mkenya.

 

Uchunguzi wa kina ulibaini kuwa mshukiwa huyo alikuwa ameandaa malipo ya KSh 100,000 kwa mshirika wake wa hapa nchini, ambaye angehusika katika utekelezaji wa utekaji nyara huo.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

 

Aidha, iligunduliwa kuwa washukiwa walipanga kuwahamisha waathiriwa hadi El-Ade kwa gharama ya KSh 300,000, kwa usaidizi wa mshirika wake wa pili, Noor Yacob Ali, mwenye umri wa miaka 29.

 

Katika operesheni nyingine iliyofanyika mapema leo, vikosi vya usalama vya pamoja vilifanikiwa kumnasa Yacob Ali katika eneo la Metameta, ndani ya Mandera township.

 

Kwa sasa, washukiwa hao wanazuiliwa na wanaendelea kuhojiwa kabla ya kufikishwa mahakamani kwa mashitaka ya kuwa wanachama wa kundi la kigaidi, kosa linaloangukia chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi (POTA).

 

Maafisa wa usalama wamewataka wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa za kutiliwa shaka ili kuhakikisha usalama unadumishwa.