Crime scene

Polisi jijini Nairobi wanamshikilia mwanamke mmoja na rafiki yake kuhusiana na kifo cha mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka minne.

 

Kwa mujibu wa ripoti ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), mshukiwa alimpeleka mtoto wake aliyekuwa amefariki katika mochari ya Hospitali ya Mama Lucy mnamo Desemba 9, 2024, akiwa ameandamana na rafiki yake.

 

Hata hivyo, baada ya kutoa taarifa kwa polisi kama walivyoelekezwa na wahudumu wa mochari, wawili hao hawakurudi tena.

 

"Kukosekana kwao kulizua shaka zaidi walipozima simu zao, hali iliyomfanya mhudumu wa mochari kuripoti suala hilo katika kituo cha polisi cha Mowlem," walisema DCI katika taarifa yake.

 

Maafisa wa upelelezi kutoka Dandora kwa ushirikiano na kitengo cha CRIB kutoka eneo la Nairobi walianza uchunguzi wa kina, ambapo walibaini ukweli wa kushtua kuhusu saa za mwisho za maisha ya mtoto huyo.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

 

Ingawa mshukiwa awali alidai kuwa mtoto alifariki usingizini, uchunguzi ulibaini kuwa alipoteza maisha kutokana na majeraha aliyoyapata baada ya kushambuliwa na mama yake kwa madai ya kujichafua wakati akijisaidia.

 

"Uchunguzi wa kina ulifichua kuwa mshukiwa ni mama mzazi wa marehemu, jambo ambalo limezidisha huzuni katika kisa hiki cha kusikitisha," DCI iliongeza.

 

Kwa sasa, mshukiwa anazuiliwa na anaendelea kusaidia maafisa wa upelelezi kubaini ukweli kamili kuhusu mauaji ya mtoto huyo.

 

“Juhudi za kutafuta haki zinaendelea, na tutahakikisha waliohusika wanawajibishwa kikamilifu kwa matendo yao,” ilisema DCI.