Shoo ya Eric Omondi na Willy Paul imefutiliwa mbali

MWANAHARAKATI Eric Omondi ambaye amekuwa katika mstari wa mbele kuandaa shoo ya msanii Willy Paul iliyotarajiwa kufanyika leo Februari 14 ametangaza kufutiliwa mbali kwa shoo hiyo.

Omondi kupitia ukurasa wake wa Facebook alitangaza taarifa hizo za kusikitisha kwa mashabiki na wapenzi wa muziki Kenya ambao walikuwa wamejiandaa kuhudhuria shoo hiyo ambayo ingefanyika hadi usiku wa manane Februari 14.

Kwa huzuni, Eric Omondi alisema kwamba kila kitu kilikuwa kinaendelea vizuri katika maandalizi ya miezi 3 ambayo yaligharimu zaidi ya shilingi milioni 21 lakini polisi walifika katika ukumbi wa KICC na kuwataarifu kwamba shoo hiyo haingeweza kufanyika.

“SIKU NYINGINE YA HUZUNI KENYA!!! Baada ya Miezi 3 ya Uwekezaji MAKUBWA, Mazoezi na Maandalizi Makali. Tukio Letu Limeghairiwa bila Sababu. Polisi wamefika KICC na kusema wana Maagizo ya Kusimamisha Tukio. Swali ni kwanini???” Eric alisema.

Omondi alieleza kwamba hata walikuwa wameitisha ulinzi wa maafisa wa polisi 50 lakini wakataarifiwa kwamba suala tata si usalama bali ni yeye ambaye hakuwa anatakikana kuandaa shoo.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Mchekeshaji huyo alionekana kutupa spana mikononi mwa serikali akiituhumu kwa kuhujumu harakati za vijana kujaribu kujikimu kupitia sanaa.

“Tuliuliza hata Polisi 50 wakasema "sio tukio, sio Usalama. Ni ERIC OMONDI na Mambo Mengine". Hii ndiyo Kenya tunayoishi. Willy Paul Aliwekeza akiba ya maisha yake kwenye hili. Over 21 Million down the drain!!!Vijana watawai inuka kweli??? IPO SIKU,” alimaliza kwa huzuni.

Eric Omondi amekuwa katika mstari wa mbele kumsaidia Willy Paul kuandaa shoo hiyo ambayo ilitarajiwa kufanyika katika ukumbi wa KICC, katikati mwa jiji la Nairobi.

Willy Paul na Eric Omondi waliibuka na wazo la shoo hiyo baada ya Pozee kudai kuhujumiwa katika hafla ya Furaha Fest Desemba 7 akidai kwamba waandaaji waliwapa kipaumbele wasanii wa kigeni kuliko wa nyumbani.

Willy Paul baada ya kuonekana kumlaumu Diamond kwenye shoo hiyo, alijitangaza kama mkombozi wa muziki wa Kenya, dhana ambayo alitarajiwa kuitetea kwa vitendo Februari 14.