Yoweri Museveni azungumzia suala la mapenzi siku ya kwanza

ZIKIWA zimesalia saa kadhaa kuelekea siku yenye umuhimu mkubwa kwa watu wanaopendana, watu mbalimbali wamejitokeza kwenye mitandao ya kijamii kueleza nini wanachofahamu kuhusu mapenzi.

Suala kuu ambalo limeonekana kuchukua mikondo tofauti ni lile la watu kusimulia jinsia walipatana na wenzi wao na kuanzisha mahusiano ya kimapenzi.

Mmoja kati ya watu ambao wamezungumzia suala la mapenzi mwezi huu wa mapenzi ni rais wa taifa jirani la Uganda Yoweri Museveni.

Katika klipu ambayo imeibuliwa mitandaoni, Museveni alionekana akieleza tamaduni ya mapenzi katika kabila lake la Ankole na kusema kwamba wao hawafahamu chochote kuhusu dhana ya watu kupendana katika kuonana kwao kwa mara ya kwanza.

Kwa mujibu wa Museveni, mapenzi katika kuonana kwa mara ya kwanza ni dhana ya watu wa mataifa ya Ulaya, akisisitiza kwamba Afrika kuna taratibu nyingi kabla ya watu kupendana.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

"Sisi katika Ankole hatuna kitu kama 'love at first sight.' Hatuingii katika upendo na watu tunaowaona sokoni. Tunasonga polepole," Museveni alisema.

“Wazungu wametuletea kitu cha hatari. Hiki ni kitu kinaitwa “love at first” sight...kwamba unaweza kuwa unatembea kwenye kituo cha mabasi na kuona mtu akipita, ukaanza kutetemeka na kupoteza moyo wako na unampenda mtu huyo papo hapo, na ndivyo hivyo!” aliongeza.

Kulingana na rais huyo, mchakato wa kutafuta mwenzi unahusisha familia kuwachunguza wapenzi watarajiwa ili kuhakikisha wanatoka katika malezi yanayoheshimika na yenye tabia njema.

"Kwanza watu wanakupendekezea mwanamke. Watakwambia hivyo na hivyo kuna binti mwenye tabia nzuri. Kisha watu wako wafanye uchunguzi wao wenyewe kuona kama ni kweli. Halafu mambo yanaenda hivyo hadi kwenye ndoa," anaeleza.

Njia hii, anasema, inasaidia kuhakikisha utangamano na utulivu katika ndoa, badala ya kutegemea hisia za muda mfupi.