
MFANYIBIASHARA ya kuuza magari, Khalif Kairo kwa mara ya kwanza amezungumzia zogo linaloendeshwa mitandaoni na baadhi ya wanablogu kuhusu uhusiano wake na Wavinya Maria.
Akizungumza na mtangazaji Brian Sakwa kwenye runinga ya Y254, Kairo alisema kwamba katika siku za hivi karibuni, baadhi ya watu mitandaoni wamekuwa wakiendeleza dhana zisizo sahihi kwamba Wavinya alimtelekeza wakati alikamatwa na polisi.
Kairo alisema kwamba Wavinya alisimama na yeye kipindi chote akiwa seli na hadi kupelekwa mahakamani kinyume na jinsi tetesi zimekuwa kwamba Mrembo huyo alimtelekeza.
Kairo alisema kwamba Wavinya alimtembelea kituoni na kumpelekea chakula na hata alikuwa anataka kuhudhuria kusikilizwa kwa kesi yake mahakamani lakini mwenyewe akamkataza.
“Kuna kitu Fulani ambacho kimekuwa kikiendelea kwenye vyombo vya habari na ambacho ninahisi kabisa si haki. Nahisi kama Wavinya amezungumziwa kwa njia hasi sana. Nahitaji kuweka wazi kitu kimoja kwenye kamera. Kusema ukweli alikuja kituoni. Ni vile tu sikuonyesha picha au video akinitembelea,” Kairo alisema.
“Kwa kweli alikuwa hata anataka kuja mahakamani lakini nilimwambia asije. Hata mamangu alikuwa anataka kuja lakini niliwaambia wasije. Unajua wakati mwingine ni sharti uwalinde kutokana na mambo hasi,” aliongeza.
Mfanyibiashara huyo alisema kwamba anahisi wanablogu wamekuwa wakimkaba shingoni aliyekuwa mpenzi wake Wavinya Maria wakidai kwamba alimkwepa wakati alitiwa korokoroni, uvumi ambao anautaja kuwa hasi.
“Wavinya alisimama na mimi. Alikuja kuniona korokoroni, aliniletea chakula, niko na meseji hapa naeza waonyesha. Hata alikuwa tayari kuja kortini lakini nilimwambia asije.”
Kairo alianza mwaka kwa masaibu ya msururu wa kukamatwa na polisi akikabiliwa na tuhuma za kutowafikishia wateja wake magari ambayo walinunua kutoka kwake.
Mwishoni mwa Januari, Khalif Kairo aliachiliwa kwa bondi ya kibinafsi ya KSh 3 milioni baada ya kukaa siku mbili mikononi mwa polisi.
Itakumbukwa pia kwamba Mnamo Januari 14, aliachiliwa kwa dhamana ya KSh 1 milioni pesa taslimu katika kesi mbili tofauti za uhalifu baada ya kukaa rumande kwa siku tatu.
Alikuwa ameshtakiwa kwa kuwalaghai wateja wake zaidi ya KSh 5 milioni kwa kujifanya angewawezesha kuwanunulia magari. Mahakama wakati huo ilizitaka pande zote kujaribu suluhu nje ya mahakama, ikisema kuwa asili ya shtaka linalomkabili Kairo ni utovu wa nidhamu.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!